Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 3:47 am

NEWS: LEMA AFURAHIA KUPELEKA USHAHIDI TAKUKURU.


ARUSHA: Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema wamefurahia kauli ya mkurugenzi mkuu wa Takukuru kuwataka kupeleka ushahidi wa tuhuma zao kuwa kulikuwa na mchezo mchafu kushawishi madiwani wao kujiunga na CCM mbele ya Rais John Magufuli katika hafla ya kiserikali iliyofanyika jijini Arusha wiki iliyopita.

Lema na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari walidai kuwa madiwani wawili wa Chadema waliotangaza kujiunga na CCM wakati wa hafla ya kukabidhi kamisheni kwa maofisa wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, walishawishiwa kwa rushwa na kwamba kitendo hicho kilifanyika katika ofisi za Serikali na wanao ushahidi usio na shaka.

Diwani mpya aliyeihama Chadema na kujiunga na CCM ni Rayson Ngowi wa Kata ya Kimandolu ambaye hata hivyo alikana kurubuniwa kufikia uamuzi huo.

Walimuomba Rais Magufuli awaite ili wampatie ushahidi huo kuonyesha kuwa kitendo hicho ni kinyume na juhudi zake za kupambana na rushwa.

Jana, Lema aliiambia Mwananchi kuwa wanashukuru mkurugenzi huyo mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola kwa kuwakaribisha kupeleka ushahidi wao.

“Tutapeleka ushahidi wetu ofisini kwake na tunaamini atafanyia kazi tuhuma hizi,” alisema.

Hata hivyo, alisema Nassari, ambaye madiwani watano wa jimbo lake wamejiuzulu, hivi sasa yuko Nairobi, Kenya kupata baraka za mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kabla ya kwenda Takukuru.

“Akirudi tutakwenda naye moja kwa moja kwa mkurugenzi mkuu wa Takukuru,” alisema

Sakata hilo lilianza wakati Rais alipokaribisha wanachama wa vyama vya siasa kujiunga na vyama vingine akisema amedokezwa kuwa wako watu waliotaka kujiunga na CCM.