- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: KOREA KASKAZINI YAFYATUA MAKOMBORA KUTOA ONYO KWA KOREA KUSINI
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un amesema makombora mawili yaliyofyatuliwa chini ya uangalizi wake Jana alhamisi Julai 26, 2019 yakifanyiwa majaribio, ni onyo kali kwa Korea kusini kuhusu mipango yake ya kufanya mazoezi ya pamoja (luteka) ya kijeshi na Marekani.
Majaribio ya makombora yaliyofanywa Alhamisi na Korea Kaskazini, yalikuwa ya kwanza tangu Kim Jong Un na rais wa Marekani Donald Trump walipokutana katika eneo lisilo la kijeshi kati ya Korea ya kusini na kaskazini na kukubaliana kuanza tena mazungumzo kati yao kuhusu silaha za nyuklia.
Makubaliano haya hayajaanza kutekelezwa, na hata kabla ya majaribio ya makombora yaliyofanywa jana, Korea Kaskazini ilishaonya kuwa huenda mazungumzo yakaathiriwa na hatua ya Marekani na Korea Kusini kukataa kuachana na luteka za kijeshi zilizopangwa kufanyika mwezi ujao.
Bila ya kutoa maelezo zaidi, shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya korea Kaskazini KCNA limetangaza kuwa majaribio ya jana, yalikuwa ya aina ya makombora mapya ya kimkakati yenye mfumo wa kiufundi ya kuyaelekeza na ambayo yalituma onyo kali kwa wachochezi wa vita wa Korea Kusini, kuhusu hatua yao ya kuendelea kukaidi maonyo na kuendelea kufanya luteka za pamoja na Marekani.
Waangalizi wa Korea Kusini wamesema kuwa makombora hayo ya masafa mafupi yaliyofyatuliwa Alhamisi yaliruka umbali wa kati ya kilomita 450 na 700 kabla ya kuanguka baharini kati ya rasi ya Korea na Japan.
Umbali huo unayawezesha makombora hayo kushambulia eneo lolote ndani ya Korea Kusini.
Kuna zaidi ya wanajeshi 30,000 wa Marekani nchini Korea Kusini, na luteka zao za kijeshi ya kila mwaka pamoja na Korea Kusini zimeendelea kuighadhabisha Korea Kaskazini.
Waziri wa ulinzi wa Japan ameutaja ufyatuliaji wa makombora hayo kuwa jambo la kusikitisha mno. Nayo ofisi ya usalama wa kitaifa ya Korea Kusini imeelezea wasiwasi mkubwa huku Marekani ikitaka matendo hayo ya uchokozi yasitishwe.
Kwa mujibu wa KCNA, Kim alisema makombora hayo ya kisasa yanaweza kuruka kilomita chache juu ya usawa wa bahari, hali inayoyafanya kuwa vigumu kuzuiwa. Shirika hilo la habari limeongeza kuwa Kim ameionya Korea Kusini dhidi ya kupuuza onyo hilo.