Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:55 pm

NEWS: KIZIMBANI KWA KUUA WATU 17 WA FAMILIA MOJA

MARA: MWANAMUME mmoja amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, kwa makosa ya mauaji ya watu 17, wote wa familia moja, wakazi wa eneo la Mugaranjabo wilayani humo, kwa kuwakata mapanga wakati wakiwa nyumbani kwao.

Ikumbukwe kuwa tukio la mauaji ya watu hao 17, na wote wakiwa ni wanafamilia moja lilitokea mwaka 2010. Aliyefikishwa katika mahakama hiyo mbele ya hakimu Richard Maganga, ametambuliwa kwa majina ya Sura Bukaba Sura maarufu kwa majina ya Phinias Yona au Epoda (35), mkazi wa wilayani Butiama mkoani Mara.

Akisomewa mashitaka yake ya mauaji ya watu 17 hao, Mwendesha Mashitaka wa Polisi Jonas Kaijage, aliiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake wapatao 15, ambao wote wakazi wa wilayani humo, walitenda makosa hayo Februari 16 mwaka 2010 majira ya usiku katika eneo la Mugaranjabo, nje kidogo ya mji wa Musoma.

Kaijage alisema mtuhumiwa huyo, alitenda kosa hilo akiwa na wenzake hao, ambao tayari walishakamatwa na kufikishwa mahakamani, ambapo kati yao wanane walikwishafariki dunia wakiwa mahabusu. Inadaiwa watu hao walimuua Kawawa Kinguye na wenzake wapatao 16, ambao wote ni wa familia moja kwa kuwakata mapanga wakati wakiwa nyumbani kwao.

Alisema kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kutekeleza mauaji hayo alitoroka, ambapo wenzake 15 walikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo. Alifafanua kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 18 mwaka huu, kwa kesi nyingine ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika eneo la Rwamulimi mjini Musoma.

Alisema katika tukio hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha, mtuhumiwa huyo alivamia nyumbani kwa mwananchi mmoja na kuvunja nyumba kwa kutumia nondo na kufanikiwa kuiba Sh 500,000 taslimu. Alisema kuwa polisi walifanikiwa kumkamata na kumtambua kuwa alishiriki katika tukio la mauaji ya watu hao 17 lililotokea mwaka 2010.

Mtuhumiwa huyo baada ya kusomewa mashitaka yake, hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusilikiza kesi za mauaji. Hakimu Karimu Moshi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 7 mwaka huu, itakapotajwa tena mahakamani hapo na kuunganishwa na washitakiwa wengine waliosalia.

Wakati huo huo, mahakama hiyo mbele ya hakimu Richard Maganga, imemhukumu Robert Kabondo (67) mkazi wa wilayani Butiama, kutumikia kifungo cha miaka saba jela, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na dawa ya kulevya aina ya bangi kinyume cha sheria.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa polisi, Kaijage kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 7 mwaka huu, kwa kupatikana na dawa hizo zenye uzito wa gramu 97.5 kinyume cha Sheria ya Kuzuia Dawa ya Kulevya Sura ya Tano ya mwaka 2015.

Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, Kaijage aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa huyo, kwani dawa za kulevya zinaharibu vijana wetu na kupunguza nguvu kazi ya taifa. Mshitakiwa huyo aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu.

Utetezi huo wa mshitakiwa huyo ulitupiliwa mbali na hakimu Maganga, ambaye alimhukumu kifungo cha miaka saba jela ili kuwa fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia au nia ya kufanya hivyo.

Source: habarileo