Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 7:22 am

NEWS: KINANA NA MAKAMBA WAMSHTAKI MUSIBA KATIKA UWONGOZI WA CCM

Dar es salaam: Vitendo vya kashifa na dharau za Cyprian Musiba, ambaye anayejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Rais John Magufuli, dhdi ya viongozi mbalimbali wa nchi, sasa zimefika mbali zaidi baada ya viongozi wakubwa kabisa waliowahi kuhudumu kwenye chama kikongwe cha utawala barani Afrika CCM kuamua kulivalia njuga na kulisemea kimaandishi dhidi ya mtu huyo.

Abdurahman Kinana, Yusuf Makamba ambao ni makatibu wakuu wastaafu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanahoji udhaifu uliokikumba chama cha CCM na serikali yake kwa kushindwa kulinda heshma yao na wananchi wengine kutokana na kuchafuliwa pia kudhalilishwa na Myu huyo anayejitambulisha kuwa ‘mtetezi wa Rais Magufuli

Makamba aliyehudumu nafasi hiyo kuanzia 2007-2011 na Kinana aliyehudumu kuanzia 2012-2018, Kufuatia kadhia hiyo, jana tarehe 14 Julai 2019 Mzee Makamba na Kinana wamemwandikia barua Mzee Pius Msekwa, Katibu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu la chama hicho, kumlalamikia kitendo cha Musiba kuwachafua viongozi wastaafu.

“Tuliamini kwamba pale anapojitokeza mtu hadharani na kuwadhalilisha viongozi waandamizi wastaafu na huku mtu huyo akijinasibisha na serikali pamoja na rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM basi hatua zitachukuliwa na taarifa kutolewa kwa umma,” inaeleza sehemu ya tamko la Mzee Makamba na Kinana.

“Kwa bahati mbaya viongozi wetu hawakuchukua hatua yoyote kuhusu jambo hilo. Na zaidi mtu huyu ameendelea kuwadhalilisha na kuvunjia heshima viongozi wastaafu na wengine katika jamii.”

"Kwa ushahidi wa kimazingira, Musiba anatumwa na wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na yeyote, zipo ishara wanaomkingia kifua wana mamlaka,baraka na kinga ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalum, kwa watu maalum, kwa malengo maovu" - KINANA NA MAKAMBA

Mzee Kinana na Makamba wametoa tamko hilo, baada ya Musiba kuwatuhumu kwa zaidi ya mara mbili, kwamba wanahusika na vitendo vya kumkwamisha Rais John Magufuli kutekeleza majukumu yake.

“Kwa sasa Watanzania wote wanajua kuwa haya anayosema mtu huyu kuhusu watu mbalimbali siyo ya kwake, yeye anatumwa kutekeleza maagizo tu na kutumika kama kipaza sauti.Huyu ni mamluki anayetumika kuivuruga CCM na nchi yetu, katika mazingira hayo hatuwezi kukaa kimya,” wamesema.

“Tunasikitika kwamba Musiba licha ya kuwatuhumu na kuwakashifu Watanzania wenzake viongozi na watendaji wa serikali, ameachwa akitamba jambo linaloashiria kwamba anakingiwa kifua , hata anapotumia lugha za vitisho na za kuhatarisha usalama wa raia hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake,” wamesema.

Makatibu hao wastaafu wa CCM wamesema wamechukua hatua hiyo badala ya kwenda mahakamani, ili wazee wa CCM watumie busara zao katika kushughulikia jambo hilo. “Tunafanya hivyo kwa kuzingatia katiba ya CCM , tumewasilisha maombi yetu tukiwasihi wazee wetu watumie busara zao katika kushughulikia jambo hili ambalo linaelekea kuhatarisha umoja mshikamano na utulivu ndani ya chama na nchi,” wamesema.