Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 4:59 pm

NEWS: KIFO CHA WAZIRI IDD CHAMKUTANISHA KINANA NA MARAIS WASTAAFU

MAMIA ya waombolezaji wakiwemo viongozi wa ngazi mbalimbali walio kazini na wastaafu katika Serikali zilizopita wameshiriki kwenye mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Baishara katika Serikali ya Awamu ya Tatu marehemu Mzee Iddi Mohamed Simba.

Mzee Simba amezikwa leo Februari 14,2020 katika makaburi ya Magomeni Mwinyimkuu jijini Dar es Salaam ambapo wakati wa mazishi hayo , Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais mstaafu Mohamed Ghalib Bilali na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi Abdulrhaman Kinana ni miongoni mwa walioshiriki kwenye mazishi hayo.

Mwili wa marehemu Iddi Simba kabla ya kupelekwa makaburini, ulioshwa katika Msikiti wa Maamur na kisha kupelekwa nyumbani kwake eneo la Mikocheni nyumba kitalu namba 109.Baada ya hapo mwili wake ulikwenda kupumzishwa kwenye makaburi hayo baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa.

Baadhi ya viongozi wamepata nafasi ya kumuelezea na kwamba enzi za uhai wake alikuwa mstari wa mbele kutoa mchango wake mkubwa kwa Taifa letu kuhakikisha linasonga mbele kimaendeleo.

Kwa upande wake aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam katika Serikali ya Awamu ya Nne Suleiman Kova amesema mzee Iddi Simba baada ya kustaafu nafasi ya Uwaziri bado aliendelea kutumia muda wake mwingi kushauri na kushiriki bega kwa bega katika shughuli za maendeleo.

Amesema kifo chake ni pigo kubwa lakini cha kujifunza ni kuangalia sifa zake lukuki ambazo zimeelezwa na waombolezaji na waliobaki hai wana kila nafasi ya kujiuliza mwisho wao utakuaje ili kuwa mfano mzuri kama aliouachwa na marehemu Iddi Simba.

"Kuna mengi ambayo yamefanywa na Iddi Simba enzi za uhai wake, sifa zake tumezisikia zikitolewa na watu ambao wamepata nafasi ya kumzungumzia, alikuwa mzalendo na mwenye mapenzi mema na nchi yetu, "amesema Kova.