Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:48 am

NEWS: KESI YA MDEE SHAHIDI AOMBWA KULETA UDHIBITISHO WA UGONJWA

Dar es Salaam. Mahaka ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imeutaka upande wa mashtaka(Jamhuri) kuleta udhibitisho wa ugonjwa wa shahidi anayedaiwa anaumwa, aliyetakiwa kutoa ushahidi mahakamani hapo katika kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Mahakama imechukua uwamuzi huo mara baada ya Wakili wa Serikali ya Tanzania, Sylivia Mitanto kudai leo Jumatatu Novemba 25, 2019 kuwa wana shahidi mmoja ambaye ni Ispekta moja alitakiwa kutoa ushahidi lakini ametoa taarifa kuwa anaumwa.

"Shauri limekuja kwa ajili ya kusikilizwa na tumemuita shahidi mmoja lakini kwa bahati mbaya ametoa taarifa tangu jana anaumwa hivyo naiomba mahakama hii iahirishe shauri hili,” amedai Mitanto.

Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Hekima Mwasipo amedai mazingira inaonyesha upande wa mashtaka hawana nia ya kuendelea na shauri hilo hivyo tunaiomba mahakama hii ifute kesi hii.

Hakimu Simba amesema shahidi wa tatu alitoa ushahidi Julai 10, 2017 hadi kufikia leo ni miaka miwili hivyo shauri hilo litakapokuja mahakamani hapo upande wa mashtaka mnatakiwa kuleta uthibitisho wa ugonjwa wa huyo shahidi.

"Haipendezi kuona shauri hili kila linapokuja mahakamani linaahirishwa kwa sababu ya shahidi kutokuwepo, hivyo mtatuletea uthibitisho wa ugonjwa wa shahidi Ispekta Moja," alisema Simba.

Hadi sasa mashahidi watatu wametoa ushahidi katika shauri hilo.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Desemba18 na 19, 2019 litakapokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Katika kesi ya msingi inadaiwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Dar es Salaam Mdee alitamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa, ‘anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,’ kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.