Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 2:20 am

NEWS: KESI YA LISSU DHIDI YA SPIKA NDUGAI KUSIKILIZWA KESHO

Kesi ya kupinga kuvuliwa ubunge iliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, itaanza kusikilizwa kesho.

Image result for lissu na spika ndugai

Jana Agosti 13, 2019 Mahakama kuu kanda ya Dar es salaam imetoa Hati ya kuwaita pande zote mbili yaani Spika Ndugai na Tundu Lissu, kufika katika mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo ambalo linalosikilizwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa.

Lissu ambaye ni Rais Mstaafu wa chama cha Mawakili Tanzania(TLS) amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, Septemba 7 mwaka juzi.

Pia chama chake cha CHADEMA kimewataka watanzania na wafuasi wa cham hicho kufika mahakamani kusikiliza kesi hiyo "Tunatoa wito kwa viongozi, wanachama, wafuasi wa Chadema na Watanzania wote wapenda haki, demokrasia na utawala bora unaoheshimu sheria, mahali popote walipo kufuatilia kwa karibu mwenendo wa shauri hilo kuanzia hatua ya sasa na kipekee kupata muda wa kufika mahakamani kuungana pamoja na kusikiliza mapambano hayo ya kuitafuta haki ya Mhe. Tundu Lissu mahakamani baada ya Spika Ndugai kutangaza kile alichodai ni kukoma ubunge wake mnamo Juni 29, mwaka huu, alipokuwa akiahirisha Bunge, Jijini Dodoma." ilisema sehemu ya taarifa ya chama hicho

Lissu alifungua shauri la maombi Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba kibali cha kufungua shauri la kupinga uamuzi huo.

Kwa mujibu wa maombi namba 18 ya mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.

Anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili iite taarifa ya uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge na kisha itengue na kutupilia mbali uamuzi huo.

Mwombaji huyo anaomba mahakama impe kibali afungue shauri ili mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika hati ya dharura, Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo, Mtaturu ambaye Julai 19, mwaka huu alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, ataapishwa kushika wadhifa huo.

Hivyo anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na masilahi yake yote yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.

Uamuzi wa kumvua ubunge ulitangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Juni 28, mwaka huu wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, huku akitaja sababu mbili.