Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 5:38 am

NEWS: KAULI YA SEREKALI KUHUSU WAFUNGWA KUPEWA TENDO LA NDOA

Dodoma: Wizara ya Katiba na Sheria, imesema kuwa suala la kuwapa nafasi wafungwa kukutana na wenza wao wakiwa kifungoni kwa Tanzania halina ulazima kwa kuwa halivunji haki za msingi za binaadamu.

Kauli hiyo imetolewa leo ijumaa Feb 8 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri Profesa Kabudi wakati akichangia taarifa za kamati za Bunge za Sheria na Sheria Ndogo kwa mwaka 2018.

Amesema Tanzania ilifanya utafiti na walibaini kuwa jambo hilo haliwezekani.

"Hata mataifa ya wenzetu huko si kwamba wenza wanakwenda magerezani hapana, bali wana utaratibu mwisho wa mwaka wafungwa wanaotembelea familia zao majumbani na kukaa hadi Januari 2 ndio wanarudi gerezani, " alisema Kabudi.

Amesema wenza wakienda magerezani hata faragha haitakuwepo kwani kila mmoja atajua wanachofanya hivyo usiri hautakuwepo huku akisisitiza uvumilivu kwani kuna wanaume rijali lakini wamekubali kuwa waseja.

Leo bungeni kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria imeishauri Serikali kuandaa na kutekeleza mpango mkakati chini ya Magereza kuwafanya wafungwa wanapata haki ya kutembelewa na wenza wao na kupata haki ya tendo la ndoa.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kamati hiyo mwenyekiti wake, Mohamed Mchengerwa amesema hatua hiyo itapunguza maambukizi ya magonjwa kwenye magereza ikiwemo Ukimwi.

“Serikali iandae na kutekeleza mpango mkakati chini ya Magereza utakaohakikisha wafungwa wenye ndoa wanawekewa mazingira yatakayohakikisha wanapata haki ya kutembelewa na wenza wao na kupata haki ya tendo la ndoa kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na mamlaka husika,” amesema.