Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 2:21 am

NEWS: KATIBU TAWALA ATENGUA MAAMUZI YA DC BARIADI

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini ametengua agizo la Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga kuchangisha fedha kwa wafanyakazi wa hospitali wa wilaya hiyo ili kununua mashine ya kupima magonjwa ya ndani mwa mwili wa binadamu (Ultra sound) iliyoibiwa

“Kuchangisha watumishi wote sio sahihi, kuna wengine walikuwa likizo na watakuwa wanaingizwa kwenye tukio ambalo pengine hawahusiki, Serikali ina vyombo vya uchunguzi, na tukio hilo ni moja ya kazi yao, Polisi ianze uchunguzi akibainika anayehusika achukuliwe hatua" amesema RAS Sagina

Mkuu huyo wa Wilaya jana alitoa agizo kuwa wafanyakazi wote waliokuwa kazini siku ambayo mashine hiyo ilipoibiwa wachangia fedha za kununua kifaa hicho kuanzia ngazi ya juu hadi chini.

Mashine hiyo iliibiwa juzi Agosti 13, 2919 katika hospitali hiyo ambapo Jeshi la Polisi Mkoni Simiyu linawashikilia watu 17 wakiwemo wauguzi wa Hospitali ya mji bariadi kwa tuhuma za kuiba Mashine hiyo.

Watu hao wanatuhumiwa kuiba Mashine hiyo pamoja na kifaa chake cha kudurufu picha (printer) ambapo ilikuwa maalumu kwa matumizi ya wodi mpya ya akina mama wajawazito na iliibiwa ikiwa kwenye wodi hiyo.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Mike Mabimbi, amekiri kuibiwa kwa mashine hiyo ambapo amesema hadi sasa bado haijapatikana.

Mabimbi amesema kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo waliweza kutoa taarifa jeshi la polisi,

“Ni kweli mashine hiyo ambayo ilitolewa na wadau wa maendeleo UNFPA kwa ajili ya wodi ya akina mama tu iliibiwa katika mazingira ya kutatinisha, tayari taarifa tulitoa na polisi wanaendelea na uchunguzi,” amesema.

Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Mwanaidi Churu, amesema mazingira ya kuibiwa kwa kifaa hicho yameendelea kuwa magumu kutokana na watoa huduma waliokuwepo wodini siku hiyo kila mmoja kudai hajui.