Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 7:56 am

NEWS: KANISA KATOLIKI KAGERA LASITISHA IBADA

Kanisa Katoliki Jimbo Katoliki la Rulenge- Ngara mkoani Kagera, limesema kuwa linasitisha ibada za misa na maadhimisho mengine yanayokusanya waumini wengi kanisani na sala za jumuiya kwa muda wa mwezi mmoja kuanzia Kesho Jumapili Aprili 19, 2020 kwasababu ya kuepuka kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Kupitia taarifa ya Askofu wa jimbo hilo, Severine Niwemugizi amesema baada ya muda uliopangwa kumalizika wataangalia hali itakavyokuwa na ikibidi muda wa kusitisha ibada utaongezwa.

“Baada ya kutafakari alama za nyakati na kujifunza kutoka kwa wenzetu Ulaya na Marekani, nchi jirani zetu na hatua ambazo Baba Mtakatifu alizichukua kwa kutoa maelekezo kwa Maaskofu Wakatoliki duniani namna ya kuadhimisha ibada katika kipindi hiki cha vita dhidi ya corona, nimebeba dhamana ya kutoa uamuzi mgumu.

“Tutaomba redio Kwizera irushe adhimisho la misa fupi ili waumini wafuatilie redioni na baada ya muda huo kumalizika tutaona hali itakuaje na ikibidi tuongeze muda tutafanya hivyo,” amesema Askofu Niwemugizi.

Aidha amewataka mapadre kuadhimisha misa peke yao kwa niaba ya waumini kuwaombea na kuiombea dunia ili Mungu atunusuru na janga hili na kuagiza sala za Jumuiya kufanyika ndani ya familia kwa familia moja moja.