Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 7:42 am

NEWS: KAMPUNI YA MANJI YALAANI UDALALI ULIOTUMIWA NA KAMPUNI YA YONO


Dar es Salaam. Kampuni ya Quality Group (QGL) limited inayomilikiwa na Yusufu Manji imelaani utaratibu uliotumiwa na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart kufunga ofisi zake, hivyo inakusudia kuchukua hatua za kisheria.

Mmiliki wa kampuni ya Quality Group (QGL)


Ofisi hizo zilizopo jengo la Quality Plaza zilifungwa siku tatu zilizopita kwa madai kuwa inadaiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA), Sh12.2 bilioni.

Mshauri Mkuu wa masuala ya sheria wa QGL, Stefano Alderighi alisema jana kuwa haamini kama kamishna wa TRA anahusika katika tukio hilo.

“Yono walipokuja tuliwaomba vitambulisho, lakini walitujibu kuwa hawana na hakuna haja ya kutupa,” alisema Alderighi.

“Hata tulipowaomba kibali cha TRA walituonyesha nyaraka ambazo hazijatiwa saini na kamishna mkuu wa mamlaka hiyo, jambo ambalo linatuaminisha kuwa huenda kamishna hafahamu chochote kuhusu watu hao.”

Alisema QGL inalaani utaratibu uliotumiwa na Yono kwanza kwa kutoonyesha vitambulisho na nyaraka zinazowapa mamlaka na pia kwa kutowapa muda wafanyakazi kuondoka ofisini na vitu vyao binafsi.

“Yono walitumia kama dakika tano tu, waliwalazimisha watumishi wote kutoka nje ya ofisi bila kuwapa muda wa kuchukua vitu vyao. Lakini pia hawakuwaheshimu wageni wa ndani na nje waliokuwa katika kituo cha afya cha kampuni ambacho nacho walikifunga,” alisema Alderighi.

Alisema tayari uongozi wa kampuni umeomba kuonana na kamishina mkuu wa TRA ili kumtaarifu suala hilo na kuomba ushauri wa namna ya kufanya kabla ya kufungua shauri dhidi ya Yono.

Pia alimuomba kamishna huyo kukifungulia kituo cha afya cha kampuni hiyo kwa kuwa hakihusiki na madai hayo ya kodi, lakini pia kwa ajili ya ustawi wa umma.

Hata hivyo, siku ambayo ofisi hizo zinafungwa, mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema wamekuwa na mawasiliano na kampuni ya Farm Equipment ambayo inamilikiwa na Manji tangu Agosti 15, lakini kulikuwa hakuna mrejesho kuhusu deni hilo.

Lakini Alderighi alisema wamewasiliana na TRA kuhusu madai yao mara mbili kabla ya tukio hilo na hata baada ya kufungiwa ofisi, wamewaandikia barua na wataendelea kushirikiana nao.

Akijibu madai hayo, mkurugenzi wa Yono, Consolata Yono alisema wanaongozwa na utaratibu kutoka TRA.

“Ni vigumu kwenda kufunga ofisi ya mtu bila kuwa na nyaraka zote muhimu. Hao kama wanadaiwa walipe tu sio kuanza kusingizia eti wameonewa,” alisema Yono.