- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: JPM: '' WAACHENI MKAPA,KIKWETE WAPUMZIKE''
DAR ES SALAAM: Rais John Magufuli amevionya vyombo vya habari, vinavyowataja Marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na kuwahusisha na taarifa za kamati mbili za uchunguzi wa madini yaliyo katika makontena yenye mchanga wa madini (makinikia), ambazo ripoti zimekabidhiwa kwake.
“Nimesoma ripoti zote mbili, hakuna mahali ambapo Mzee Mkapa na Mzee Kikwete wametajwa, vyombo vya habari viache kuwachafua hawa wazee, wamefanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa letu, viwaache wapumzike,” alisema Rais Magufuli.
Gazeti la Tanzania Daima katika ukurasa wake wa kwanza toleo la jana, lilikuwa na habari kuu yenye kichwa cha habari kisemacho “Wakamatwe’, wabunge wawacharukia Mkapa, JK waondolewe kinga”.
Habari hiyo iliambatana na picha kubwa za Mkapa na Kikwete Kwa upande wake, gazeti la Nipashe toleo la jana, lilikuwa na habari kuu ukurasa wa kwanza yenye kichwa cha habari kisemacho “Wataka Mkapa, JK washitakiwe” ni katika sakata la makinikia.
Habari hiyo kuu iliambatana na picha kubwa za Mkapa na Kikwete. Wakati huohuo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema kuwa analipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake jana asubuhi wa kuacha kuwashambulia ndani ya Bunge viongozi wetu (marais wastaafu) hao, walioitumikia nchi yetu kwa miaka mingi na kutufikisha kwenye amani na usalama tulionao leo.
Bunge lilifikia uamuzi huo kwa mujibu wa Ibara ya 46 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayowapa kinga viongozi hao na Kanuni ya 64 ya Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zinazozuia mijadala isiyo na mipaka.
“Ikumbukwe kwamba taarifa iliyotolewa na kamati haikuwataja wala kuwatuhumu marais hao wastaafu. Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli inawaheshimu marais wastaafu na kutambua mchango wao adhimu katika kujenga ustawi wa nchi yetu.
“Kutokana na msingi huo, naviasa vyombo vya habari nchini na mitandao ya kijamii, kuacha mara moja muelekeo huo hasi, ambao una kila dalili ya kututoa kwenye mstari na kupotosha kampeni tuliyonayo ya kujikomboa kiuchumi,” alisema Waziri Mwakyembe.
Mapema jana, Kiti cha Spika kilizuia kuwajadili marais wastaafu bungeni, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu aliwaambia wabunge akijibu Mwongozo wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, kuwa wabunge wanapaswa kuacha kuwajadili marais hao wastaafu, kwani wana kinga kwa mambo waliyoyafanya wakiwa madarakani, sawa na Rais aliyeko madarakani.
Mkapa alikuwa Rais wa Awamu ya Tatu kutoka mwaka 1995 hadi mwaka 2005 na Kikwete alikuwa Rais wa Awamu ya Nne kutoka mwaka 2005 hadi 2015, alipomwachia kijiti Rais Magufuli.
Rais wa Awamu ya Kwanza alikuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyeongoza nchi kutoka 1961 hadi 1985 na kufuatiwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi mwaka 1985 hadi 1995.