Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 9:42 am

NEWS: JESHI LA POLISI LAKAMATA BUNDUKI 4

DAR ES SALAAM: JESHI la Polisi mkoani Pwani limekamata bunduki nne zilizokuwa zikitumiwa na wahalifu pamoja na dawa za kulevya.

Akizungumza na askari wa vitengo mbalimbali vya jeshi hilo mjini Kibaha baada ya gwaride la ukakamavu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Jonathan Shanna, alisema silaha hizo na dawa za kulevya vilikamatwa katika doria zinazoendelea mkoani humo.

Shanna alisema silaha hizo zimekamatwa katika wilaya mbalimbali za mkoa huo na kwenye matukio mawili tofauti, watu wanaodhaniwa kuwa majambazi walikurupushwa na kuziacha. “Tukio la kwanza lilitokea eneo la Msufini Mlandizi wilayani Kibaha.

Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walikurupushwa na polisi na kuangusha silaha aina ya shotgun ambayo haikuwa na namba,” alisema Shana. Alisema kuwa tukio la pili ambalo watu hao waliangusha silaha lilitokea eneo la Bungi Mkuza baada ya watu wanaodhaniwa kuwa majambazi kukurupushwa na kutelekeza silaha aina ya Rifle Mark IV 458 ikiwa imekatwa kitako.

“Pia tumefanikiwa kukamata silaha aina ya shotgun moja yenye namba za usajili 68687 huko wilaya ya Bagamoyo katika operesheni za kukamata wahalifu,” alisema Shanna. Aidha alisema walifanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya heroin gramu 1.20 na bangi kilogramu 1.07 huko Chalinze wilayani Bagamoyo.