Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 3:50 am

NEWS: JESHI LA POLISI LADHIBITISHA KUMSHIKILIA TITO MAGOTI

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam nchini Tanzania limedhibitisha kuwa linamshikilia Ofisa wa kitengo cha Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti pamoja na watu wengine watatu kwa uchunguzi na mahojiano zaidi.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa jioni Desemba 20, 2019 na Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa imesema Magoti (26) ambaye ni Mkazi wa Ubungo Kibo, Dar es Salaam hakutekwa bali amekamatwa yeye na watu wengine watatu aliokuwa nao.

Amesema Magoti na wenzake amekamatwa na Polisi wa kanda hiyo leo Ijumaa saa 5 asubuhi maeneo ya Mwenge na yupo katika mikono salama na wote kwa pamoja wanaendelea kuhojiwa kwa tuhuma za makosa ya jinai.

“Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada ya kukamilisha uchunguzi na mahojiano.”

“Baada ya kukamatwa mtuhumiwa huyo tumesikia taarifa mbalimbali zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ametekwa, tunapenda kuutaarifu umma kuwa hajatekwa na hakuna matukio ya utekaji ndani ya Jiji la Dar es Salaam na hali ya ni shwari kabisa,” amesema Mambosasa