Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 2:28 pm

News: Jengo jipya la Mwananyamala litasaidia kupunguza msongamano wodi ya mama na mtoto

DAR ES SALAAM: Jengo jipya la ghorofa tano linalojengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwananyamala litasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza msongamano katika wodi ya mama na mtoto.


Mganga Mfawidhi wa Mwananyamala, Dk. Daniel Nkungu amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo.


Dk. Nkungu amesema pamoja na kwamba jengo hilo ni mahususi kwa ajili ya mama na mtoto pia litakuwa na wodi maalum za huduma za private kwa ajili ya wagonjwa wengine.

“Tunakabiliwa na changamoto ya nafasi hasa kwa wakina mama, tumetenga wodi sita kwa ajili ya mama na mtoto lakini bado hazitoshi.


“Kwa mwaka tunapokea wajawazito wanaohitaji huduma ya kujifungua wapatao 12,000, idadi hii ni sawa na wajawazito 1,000 kwa mwezi, kipindi chenye idadi kubwa zaidi huwa ni April hadi Juni,” amesema.

“Tulihitaji kupata vitanda 200, tunashukuru kwamba jengo hili litakapokamilika tutapata ahueni kubwa kwani tutaongeza 100, hivyo tutakuwa tumeweza kupunguza changamoto inayotukabili,” amesema Dk. Nkungu.

Akizungumza, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemtaka Makandarasi wa kampuni ya Ujenzi MISTECO, anayejenga jengo hilo kuhakikisha anakamilisha ujenzi mapema na kulikabidhi ifikapo Desemba 30, mwaka huu.


Amesema awali mkandarasi huyo alikusudia kukamilisha ujenzi huo hadi kufikia April, mwakani.

RC Makonda amemtaka mkandarasi huyo kufanya kazi mchana na usiku kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kwa muda aliomtaka.

“Ujenzi wa jengo hili ulianza 2014 hata hivyo lilikwama, mwaka huu ujenzi umeanza tena, baada ya kumueleza Rais John Magufuli changamoto ya wodi, wakina mama wanabanana na kulala chini.

“Kupitia Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Rais Magufuli aliridhia kuipatia Mwananyamala Sh. Bil 2.1 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huu,” amesema.

Ameongeza "Sasa mkoa huo unafanya vizuri katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu na afya na kwamba sasa anakusudia kuanza kutoa tuzo maalum kutambua mchango wa watumishi.

“Sekta ya afya inazidi kufanya vizuri, wapo madaktari wanaongoza kufanya upasuaji, watu wanakuwa wazima, wengine wanawasaidia wakina mama kujifungua salama hata idadi ya vifo vya mama na mtoto imepungua kwa kiasi kikubwa katika mkoa huu.

“Kwa msingi huo, tutaanza kutoa tuzo kwa walimu na wataalamu wa sekta ya afya kwa kazi kubwa wanayoifanya, kama ambavyo tunafanya kwa Jeshi la Polisi,” amesema.

RC Makonda ameongeza “Kwa mwaka jana pekee takwimu zinaonesha zaidi ya watu mil. 6.8 walikuja kutibiwa mkoa huu, wakina mama waliojifungua walikuwa zaidi ya 126,000.

“Hii ni picha njema kwamba hata katika sekta ya afya tunafanya vizuri, wengi wanaotoka katika mikoa jirani wanakimbilia kwetu kupata huduma za afya,” amesisitiza.

Amesema sambamba na hilo, hivi sasa yupo katika mchakato wa kupata wadau kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya huko Kawe, Bunju na kukamilisha hospitali ya Wilaya inayojengwa huko Mabwe Pande.

Mkandarasi wa jengo hilo wa Kampuni ya MISTECO inayomilikiwa na chuo kikuu cha sayansi na teknolojia Mbeya (MUST), Moses Moyo, amemhakikishia RC Makonda kwamba watajitahidi kukamilisha ujenzi ndani ya muda huo.