Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 4:08 pm

NEWS: JAMHURI YAOMBA MUDA WA KUWAJIBU WADHAMINI WA LISSU

Dar es Salaam . Upande wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi inayomkabili aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu umeomba muda wa kutosha kupitia na kujibu maombi ya kujitoa kwa wadhamini wa Rais Mstaafu wa TLS.

Maombi hayo yamewasilishwa leo Ijumaa Februari 21, 2020 na wakili mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon.

wakili huyo wa upande wa mashtaka alieleza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kutokana na wadhamini wa Lissu kuwasilisha maombi hayo, hawakupata muda mzuri wa kuyapitia.

"Hivyo, kwa sababu hiyo tunaiomba mahakama itupe muda wa kutosha wa kupitia maombi hayo ili na sisi tuweze kuandaa kiapo kinzani na kuwasilisha mahakamani hapa.”

"Katika maombi ya wadhamini, wameweka vitu vingi, hivyo kama upande wa mashtaka tunahitaji tupewe muda wa kutosha ili tuweze kupitia maombi yao,” amesema.

Lissu na wenzake wanaokabiliwa na mashtaka matano likiwemo la uchochezi, hajatokea mahakamani tangu aliposhambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017 mjini Dodoma.

Siku hiyo alipelekwa Hospitali ya Mkoa ya Dodoma na usiku akahamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na baadaye kwenda Ubelgiji kumalizia matibabu. Lissu amepona lakini bado yupo nchini Ubelgiji kwa maelezo kuwa anataka kuhakikishiwa usalama wake kabla ya kurejea Tanzania.

Kutoonekana kwake mahakamani kumesababisha shauri hilo kuzorota huku wadhamini wake wakiomba kujitoa.

Wakati upande wa mashtaka ukiomba muda zaidi ili uweze kupitia maombi ya wadhamini hao, wakili wa Lissu aliiomba mahakama hiyo iahirishe kusikiliza maombi hayo hadi Februari 24, 2020.

Akimwakilisha Peter Kibatala, wakili Rwekama Rwekiza amesema kwa kuwa Kibatala yupo Mahakama ya Rufani katika kesi nyingine, anaomba iharishwe kwa muda mfupi hadi Jumatatu, siku ambayo atakuwepo.

Lakini baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Simba ameahirisha shauri hilo la hadi Machi 10, 2020.