Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 3:41 pm

NEWS: JAFO AWAONYA WAKANDARASI WASHAURI WA MIRADI YA MAJI.

DODOMA: NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo amesikitishwa na baadhi ya wakandarasi washauri wanaosimamia miradi ya maji katika halmashauri mbalimbali hapa nchini kwa kutofanya kazi yao kwa umakini na hivyo kuruhusu wakandarasi wa ujenzi wa miradi ya maji kujenga miradi hiyo chini ya kiwango.

Jafo alitoa kauli hiyo alipotembelea mradi wa maji katika kijiji cha Mkoyo ndani ya Manispaa ya Dodoma, ambapo amebaini mkandarasi mshauri wa mradi huo O&A Co LTD hakuwa makini wakati wa utekelezaji wa mradi huo kwani imeonekana mradi huo ukiwa na changamoto kadhaa licha fedha nyingi kutumika zaidi ya milioni 430 kati ya milioni 480 zilizipangwa kwa mradi huo.

Alisema wakandarasi hao wamekuwa wakisababisha miradi kujengwa chini ya kiwango na kusababisha kushindwa kuwapatia maji wananchi kama ilivyotarajiwa.

Aidha alibaini kampuni hiyo mshauri huyo ndiye yule yule aliyesimamia mradi kijiji cha Itiso ambao aliutembelea mradi huo mwezi Agosti mwaka huu na kukumbana na changamoto nyingi.

Kufuatia hali hiyo, Jafo alimuagiza Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Rais Tamisemi Mhandisi Enock kwa shirikiana na wahandisi wa maji wa halmashauri za mkoa wa Dodoma kufanya tathmini ya miradi yote ya maji inayosimamiwa na mshauri huyo ili Ofisi ya Tamisemi ifanye maamuzi sahihi.

Aidha alisema serikali haitaweza kuvumilia endapo ikibainika mshauri wa miradi hiyo ameshindwa kuisaidia serikali katika miradi ya maji anayoisimamia.