Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:41 pm

NEWS: JAFO AKEMEA TATIZO LA MIMBA KWA WANAFUNZI

MWANZA: Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo amekemea tatizo la wanafunzi wa sekondari kupata mimba wakiwa shuleni ambapo hadi sasa kuna wanafunzi 108 ambao wamebainika kuwa na ujauzito kwenye wilayani Ukerewe.

Kauli hiyo ameitoa katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali wilayani humo.

Jafo amewataka viongozi wote wilayani humo kuungana kupambana na tatizo hilo bila ya kuoneana aibu.

Naibu Waziri huyo amewataka wanafunzi kuzingatia masomo kwani elimu ndio msingi wa maisha kwa mwanadamu yeyote.

Amewakemea wanafunzi wakike wenye tabia ya kujihusisha kwenye mapenzi wakiwa na umri mdogo na kwamba jambo hilo linahatarisha mustakabali wa maisha.

Katika ziara hiyo,Jafo alifanya ukaguzi wa ujenzi wa mabweni, madarasa, maabara, na vyoo kwa shule ya sekondari Pius Msekwa na sekondari ya Bukongo ambapo serikali ilipelekwa fedha mwezi April mwaka huu zaidi ya sh. milioni 500 ili kuwezesha elimu ya kidato cha tano na sita wilayani humo.

Naibu Waziri Jafo amemaliza ziara yake wilayani Ukerewe mkoani Mwanza na kuelekea wilaya na Tarime na Rorya mkoani Mara.