Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 7:44 am

NEWS: IGP SIRRO AWATAKA WANASIASA KUACHA KUINGILIA KAZI ZA JESHI LA POLISI.

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Nyakoro Sirro amefunguka na kuwataka wanasiasa nchini kuacha kuingilia kazi ya jeshi la polisi ikiwepo upelelezi wa tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.


IGP Sirro amesema hayo siku moja baada ya viongozi mbalimbali wa upinzani kutoa kauli kuhusu jeshi hilo la polisi na kusema kuwa hawana imani na uchunguzi ambao unafanywa na jeshi hilo dhidi ya tukio la kupigwa risasi kwa Mbunge Tundu Lissu Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma.

Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, Godbless Lema wa Arusha pamoja na Mbunge wa Rombo Mhe. Joseph Selasini ni kati ya wabunge ambao walionyesha kusikitishwa na kauli ambayo aliitoa IGP Sirro akiwa mkoani Mtwara kuhusu uchunguzi wa sakata la Tundu Lissu na kusema kuwa dereva wa Lissu anachelewesha upelelezi wa sakata hilo.

Wabunge hao walikwenda mbali zaidi na kusema wao wanaona jeshi la polisi halihitaji kufanya uchunguzi wa kina juu ya sakata hilo kwa kuwa jeshi hilo linafahamu nini kipo nyuma ya tukio la kupigwa risasi kwa Tundu Lissu akiwa mjini Dodoma. Kufuatia kauli hizo IGP ndipo amefunguka na kuwataka wanasiasa kuacha kuingilia kazi ya jeshi la polisi ikiwa pamoja na uchunguzi wa sakati hilo.