Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 12:58 pm

NEWS: IDRIS SULTAN AKAMATWA NA KUACHIWA KWA DHAMANA

Dar es Salaam. Msanii wa vichekesho na mshindi wa mashindano ya Big Brother Afrika 2014, Idris Sultan leo Alhamisi Oktoba 31, 2019 amehojiwa kwa saa tano katika kituo cha polisi cha kati(Central Polisi) Jijini Dar es salaam.

Mara Baada ya mahojiano, msanii huyo alikwenda na polisi nyumbani kwake na kufanyiwa upekuzi.

Alitakiwa kwenda polisi na mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda jana baada ya kuweka picha yenye sura yake huku akiwa ameketi katika kiti chenye nembo ya Taifa.

Pia, Idris aliweka picha nyingine inayoonyesha sura ya Rais John Magufuli akiwa amesimama huku amevaa suruali yenye mikanda inayoshikizwa mabegani (suspenda).

Hata hivyo, dakika chache baada ya Makonda kumtaka msanii huyo kuripoti polisi, waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliahidi kumuwekea dhamana iwapo angekamatwa.

Eliya Rioba, mwanasheria wa mchekeshaji huyo amesema kuwa alipigiwa simu asubuhi akitakiwa kumfikisha mteja wake kituo hicho cha polisi kwa mahojiano.

“Walimpigia Sultan hawakumpata, wakampigia meneja wake Dokta Ulimwengu ambaye aliwapa namba zangu na wakanipigia. Nimekwenda naye saa 5 asubuhi na tumehojiwa hadi saa 10 jioni,” amesema Rioba.

Amesema katika upekuzi huo, polisi wamechukua kompyuta mpakato kwa ajili ya uchunguzi, kwamba walipofika kituoni walipelekwa kitengo cha makosa ya mtandaoni.

“Ameshikiliwa kwa makosa mawili, la kujifananisha na mtu mwingine na kuchapisha taarifa za uongo. Makosa ambayo yameainishwa kwenye kifungu namba 15 na 16 vya sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015,” amesema Rioba.

Ameongeza, “muda huu (saa 12 jioni) tunarudi kituoni, ninakwenda kushughulikia taratibu za dhamana ikiwezekana atoke leo.”

Kamanda wa polisi mkoa wa Ilala, Zuberi Chembela alipoulizwa kuhusu kushikiliwa kwa mchekeshaji huyo amesema, “mpigie Kamanda Mambosasa kwa sababu issue yake imetoka Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, wao wanaweza kuwa na majibu.”