- BREAKING NEWS: TANZANIA YAKANUSHA KUWASHIKILIA KINA DR SLAA NA MWAMBUKUZI
- BREAKING NEWS: RAIS WA MAPINDUZI WA NIGER AMTEUA WAZIRI MKUU MPYA
- BREAKING NEWS: SHILINGI YA KENYA YAPOROMOKA VIBAYA DHIDI YA DOLA
- BREAKING SEREKALI YA RWANDA YAKASIRISHWA NA UBELGIJI KUTOMUIDHINISHA BALOZI WAKE
- BREAKING NEWS: RAIS KIM AKUTANA NA WAZIRI WA ULINZI WA URUSI
NEWS: HOSPITALI YA BMH KUZINDUA MAABARA MAALUMU YA UPASUAJI WA MAGONJWA YA MOYO.
DODOMA: Hospitali ya Benjamin Mkapa(BMH),kesho inatarajia kuzindua rasmi maabara ya upasuaji magonjwa ya moyo ikiwemo matundu na kuziba kwa mishipa.
Akizungumza leo na waandishi wa habari kuhusu kuanza kutolewa kwa huduma hiyo, Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo katika hospitali hiyo, Dk.Wilfred Rutahoile alisema wameanza kufanya uchunguzi na kuzibua mishipa ya damu na tayari wagonjwa wawili wamechunguzwa.
“Wagonjwa hawa walikuwa wanasumbuliwa na matatizo ya kifua kwa muda mrefu na wamekuwa wakihudhuria kliniki hapa lakini bado maumivu yalikuwa yakiendelea, tukaamua kuanza kufanya uchunguzi wa mishipa yao ambapo tumefanya,”amesema.
Amebainisha kuwa kwa siku ya leo watawafanyia wagonjwa saba upasuaji huo na wataendelea kutoa huduma hiyo hospitalini hapo.
“Kwasasa tupo na madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Jakaya Kikwete(JKIC) kwasababu mashine ni mpya na imekuwepo muda mrefu bila kufanya kazi, kwasababu wao wana uzoefu wamekuja hapa ili kufanikisha kufanyika kwa ufanisi zaidi,”amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dk.Alphonce Chandika amesema maabara hiyo imeanza kufanya kazi na mashine inayotumika kufanya upasuaji huo imegharimu takribani Sh.Bilioni tano.
“Huu mtambo ni wa kisasa na hapa hospitali tayari tuna wataalam watatu, serikali iendelee kuleta wataalam zaidi ili kudumia wananchi, kwa hapa nchini hii ni maabara ya tatu lakini mashine iliyopo hapa ni ya kipekee kwa kuwa una uwezo wa kufanya huduma ya mishipa mingine ya kichwa hata ya miguu,”amesema.
Hata hivyo amesema kuanza kutoa huduma hiyo na huduma mbalimbali za figo kutawezesha kupata wagonjwa kutoka nje ya nchi.
“Tuna mashine ya uvunjaji mawe kwenye figo ambayo ni mashine ya kipekee nchini, tunashukuru sana Rais John Magufuli kwa kuwajali wananchi wake,”amesema.
Naye, Mkurugenzi wa taasisi ya JKCI,Prof.Mohamed Janabi amesema wamefika katika hospitali ya Benjamin kusaidiana na madaktari kutoa huduma hiyo ambayo itawafanya wananchi wasisafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo jiji la Dar es salaam.
“Mgonjwa wa kwanza anatokea Maswa na mgonjwa wa pili anatokea Singida kati yao yupo mgonjwa hakimu, mwanasheria,”amesema.
Mkurugenzi huyo amesema hatua hiyo itapunguza foleni katika taasisi hiyo ambayo kwa mwaka jana iliwafanyia upasuaji zaidi ya wagonjwa 1000.
“Tutapanga utaratibu wa sisi kuwepo hapa ili wataalamu wa hii hospitali wapate utaalam kama wetu ambao tumeanza kutoa huduma hii miaka mitatu iliyopita,”amesema.
Amesema kwa miaka mitatu wamehudumia wagonjwa takribani laki mbili wa magonjwa mbalimbali ya moyo hivyo ni tatizo kubwa.
“Taasisi ya JKCI tunaona wagonjwa kila siku kati ya 250 hadi 300 wa ndani, na tunafanya upasuaji kati ya wagonjwa 8-10 kwa siku, upasuaji wa kusimamisha moyo kati ya mgonjwa mmoja hadi wawili kwa siku,”amesema.