Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 6:50 am

NEWS: HICHI NDICHO KILICHOMLAZA LISSU RUMANDE

DAR ES SALAAM: Mbunge wa Singida Mashariki, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha CHADEMA Mheshimiwa Tundu Lissu, amekamatwa na Mlinzi wa amani alipokuwa anatoka mahakamani Kisutu .

Wamesema wamemkamata kwa ajili ya mahojiano.

"Tumetoka Mahakama ya Kisutu muda huu ambapo Mwanasheria Mkuu wa Chama, Tundu Lissu alikuwa na kesi ya tuhuma za uchochezi (uchochezi one) lakini pia alikuwa ni wakili kwenye kesi inayomkabili Yericko Nyerere hapa hapa Kisutu.

Wakati gari la Lissu likiwa liko getini tayari kwa kutoka, likawa blocked na nyuma ya gari yake pia likasimama gari jingine likiwa na askari polisi wenye silaha, kisha wengine wakamfuata na kumwambia yuko chini ya ulinzi na atakiwa kwenda Central Police.

Wakamtaka ashuke kwenye gari lake na apande gari jingine la kwao kwa ajili ya kuelekea Central Police". Amesema Makene.

Lissu alikamatwa mida ya 13:30hrs, lakini Mpaka Sasa bado Lissu anashikiliwa na Polisi Katika kituo kikuu cha kati na mawakili waliopo bado hawajajibiwa kama atapata dhamana ama laaa. ....tutawajuza kadiri ya taarifa zinavyokuja.

Mwanasheria mkuu wa Chama Tundu Lissu anatuhumiwa kwa kosa la kutaja makosa ya rais hadharani na uchochezi kuhusu ndege aina ya bombardier Q400.

Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA Tundu Lissu amehojiwa kwa tuhuma za kufanya makosa mawili;

1. Kumkashifu rais.

2. Uchochezi kuhusu kuzuiliwa na kushikiliwa kwa ndege ya serikali ya bombardier.

Makosa hayo yanadaiwa kufanywa kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ijumaa iliyopita, Agosti 18, mwaka huu.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, amekataa kutoa maelezo yoyote polisi, akitumia haki yake ya kisheria kuwa mtuhumiwa ana haki, kisheria, kutaja jina na anuani yake tu anapokuwa anashikiliwa na polisi hadi atakapopelekwa mahakamani ambako ndiko atataoa maelezo kujibu mashtaka anayotuhumiwa nayo.

Lissu ambaye ameendelea kuwa imara akiwa tayari kujibu mashtaka yake mahakamani, akiwa polisi amepata msaada wa kisheria kutoka kwa Wakili Faraji Mangula, ambaye pia anashughulikia uwezekano wa mteja wake kupata dhamana kwa mujibu wa sheria.

Chama kimeshatoa maelekezo kwa wanasheria wa chama kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi za kisheria iwapo Jeshi la Polisi halitampeleka mbele ya mahakama Lissu ndani ya muda unaoagizwa na sheria za nchi yetu.

Aidha, chama kinaendelea kusisitiza kuwa serikali bado inao wajibu wa kujibu hoja za msingi zilizotolewa na Chama kupitia tamko lililosomwa na Mwanasheria Mkuu wa Chama Lissu kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu kushikiliwa kwa ndege ya Tanzania huko nchini Canada kwa sababu ya deni tunalodaiwa kama nchi la shilingi bil. 87.

Tunaikumbusha serikali kuwa mojawapo ya hoja zilizotolewa na chama katika tamko hilo ni pamoja na;

1. Kwanini Serikali, kupitia kwa Waziri wa Ujenzi wa wakati huo, John Magufuli ilivunja mkataba wa Kampuni ya Stirling Civil Engeering Ltd? Kitendo ambacho kimesababisha nchi yetu kuingizwa hasara kwa kudaiwa mabilioni ya shilingi.

2. Kwanini deni la Stirling Civil Engeering Ltd halikulipwa mara baada ya mahakama ya usuluhishi kutoa tuzo ya dola za Marekani mil. 25, kitendo ambacho kimesababisha deni hilo sasa kufikia dola mil. 38.711?

3. Wananchi wanataka kujua katika kashfa hiyo ambayo ni dhahiri inalitia doa na aibu kubwa taifa letu kuwa halizingatii sheria na taratibu katika uendeshaji wa masuala yake, NANI atawajibika kijinai kwa kulisababishia taifa letu hasara ya bilioni 87?

4. Je serikali hii ya CCM ambayo imekuwa ikijigamba kuwa inao uwezo wa kutumbua majipu, je itaweza kutumbua hilo?

Leo ikiwa ni siku ya tano tangu CHADEMA kilipotoa hadharani tamko hilo kuhusu kashfa hiyo ya kuzuiliwa kwa ndege hiyo ya Bombardier huko Canada, Serikali haijajibu hoja zilizotajwa hapo juu kwa ukamilifu wake. Ni vyema serikali ikatoa hadharani na majibu yenye hoja badala ya kutaka kupindisha kwa kumkamata na kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Chama, Tundu Lissu ambaye alisoma tamko hilo mbele ya viongozi wakuu wa chama kwa niaba ya wanaCHADEMA nchi nzima.

Makene