Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 3:38 am

NEWS: HALMASHAURI YA GAIRO YATEKELEZA MAAGIZO YA SERIKALI YA UJENZI WA MAJENGO YA OFISI.

MOROGORO: Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tamisemi Mhe. Selemani Jafo amewapongeza halmashauri ya wilaya ya Gairo mkoani Morogoro kwa kutekeleza maagizo ya serikali kwa maendeleo mazuri ya ujenzi wa majengo ya Ofisi ya halmashauri hiyo.

Jafo Ametoa pongezi hizo Leo alipokuwa akiweka jiwe la msingi la jengo hilo la kisasa ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75.

Ujenzi huo umetokana na agizo alilolitoa Agosti 17, mwaka huu, alipotembelea jengo la la halmashauri ya Chamwino mkoani Dodoma na kuagiza halmashauri yeyote ambaye imepewa fedha za ujenzi wa Ofisi lakini zitakuwa hazijaanza ujenzi baada ya mwezi mmoja baada ya tarehe hiyo zingenyang'anywa fedha hizo na kupelekwa katika halmashauri ambazo wanaendele na ujenzi.

Akizungumza katika uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Gairo iliyopo mkoani Morogoro, Jafo amesema halmashauri hiyo imekuwa ya mfano kwa kutekeleza maagizo yake.

Amesema halmashauri hiyo imeamua kujichimbia kwenye ujenzi huo kwa kutumia mkandarasi Pacha Construction Company ambaye amefanya kazi kubwa na nzuri ndani ya muda mfupi.

Hata hivyo, Naibu Waziri Jafo amewaagiza makatibu Tawala wa mikoa yote ambayo halmashauri zao zilipatiwa fedha lakini bado hawajaanza ujenzi mpaka sasa wawasilishe majina ya halmashauri hizo kabla ya Oktoba 10, mwaka huu ili mchakato wa kuzihamisha fedha hizo ufanyike mara moja kwa kuzipeleka fedha hizo katika halmashauri zinazo endelea na ujenzi kwasasa.

Jafo anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kubaini hatua za utekelezaji wa miradi hiyo na kupima kama miradi hiyo inazingatia thamani ya fedha.

Katika hatua nyingine, Jafo amekagua ujenzi wa barabara za Gairo mjini huku akimhimiza meneja wa wakala wa barabara vijijini(Tarura) kuhakikisha anasimamia ujenzi huo ili ifikapo mwaka 2019 ahadi zote alizozitoa Rais Dk.John Magufuli katika barabara za halmashauri hiyo ziwe kukamilika.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 3.5 inajengwa na mkandarasi C.G.I contractors LTD.

Akikagua barabara hiyo amewahakikishia wananchi kuwa serikali itafanya jitihada katika kuhakikisha barabara zinajengwa na kwa kiwango kinachotakiwa na kutoa fedha kwa wakati ili mkandarasi aliyepo aweze kumaliza kazi kama ilivyopangwa.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo mkandarasi Stephen Aloyce amesema ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 70 na kuiomba serikali kukamilisha malipo ya shilingi Bilioni 1.5 ili kumalizia kazi iliyobaki kabla ya kipindi cha mvua kuanza.

Awali akizungumza na watumishi kabla ya kukagua barabara hiyo, Jafo amesema kutokana na taarifa ya ukaguzi iliyotolewa halmashauri hiyo ni moja ya halmashauri 6 zilizofanya vibaya katika mfuko wa barabara jambo ambalo linapaswa kusimamiwa vizuri kwa sasa ili lisijirudie tena.

"Taarifa ya ukaguzi inaonyesha Gairo ni moja ya halmashauri 6 zinazofanya vibaya,hili hatutalivumilia,taarifa hiyo ipo nitaiangalia na kama kuna mtu alishiriki katika hilo hata kama hayupo hapa tutamchukulia hatua,"amesisitiza Jafo.

Amewataka kuwa makini na ubora wa barabara zinazojengwa kulingana na thamani halisi ya miradi hiyo ili barabara zinazojengwa zisije kuharibika baada ya muda mfupi.

Naye, Mbunge wa jimbo la Gairo Ahmed Shabiby ameishukuru serikali kwa jitihada zake za kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi huku akiiomba serikali kuwasaidia kutatua kero ya maji ambayo bado inawaumiza wananchi hao.