Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 7:37 am

NEWS: HALIMA MDEE AUJIA JUU MUSWADA WA SHERIA BUNGENI

Dodoma: Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ameoneshwa kukasirishwa na muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2018 huku akisema baadhi ya vipengele vya muswada huo vinavunja Katiba.

Kauli hiyo ameongea leo Bungeni wakati akichangia muswada huo aidha Mdee amesema miongoni mwa kinachovunja Katiba ni kile kinachompa mamlaka msajili wa vyama vya siasa kukifuta chama ambacho kitashindwa kuwa na kumbukumbu za wanachama wake.

“Muswada huu unataka vyama vya siasa viweke rejista kila ngazi. Kuna wanachama wanaingia na wanatoka kila siku na kununuliwa kila leo.

Sasa chama kitakuwa hakina kazi nyingine zaidi ya kuweka kumbukumbu,” amesema. Amesema muswada huo unasema kuwa chama kitakachoshindwa kufanya hivyo msajili atakifuta lakini Katiba inasema mazingira ambayo inaweza kukinyima chama usajili ama kukifuta.

Mdee amependekeza kifungu hicho cha 8 (C) kifungu kidogo cha 3 kifutwe kwa kuwa kinakwenda kinyume na Katiba. Amesema ibara ya 13 ya Katiba inasema ni marufuku kufanya ubaguzi lakini baadhi ya vifungu vya muswada huo vinakwenda kinyume

“Uvunjwaji wa Katiba si jambo dogo. Tunataka ufanye marekebisho utakapokuja hapa (Waziri katika ofisi ya waziri mkuu sera, bunge, vijana, kazi, ajira na watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama)” amesema. Mdee amesema kifungu kingine wanachokitaka kifutwe ni kinachohusu zuio la vikundi vya ulinzi: “Hakuna asiyefahamu kuwa vikosi vya ulinzi wakati wa uchaguzi vimekuwa vikifanya kazi ya CCM. Polisi wanalinda maboksi ya kura. Kusingekuwa na shida kama majeshi yangesimama katikati.”