Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 9:50 am

NEWS: HALIMA MDEE APOKEA WITO WA KIMAANDISHI KUHOJIWA KAMATI YA MAADILI

Mbunge wa Kawa (CHADEMA) Halima James Mdee hatimaye amepokea wito rasmi wa Spika wa Bunge Job Ndugai wa kutaka kuhojiwa na Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge juu ya maneno yake ya kuunga mkono kauli ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serekali (CAG) Prof. Mussa Asaad.

Tokeo la picha la halima mdee na spika

Januari 7, 2019 Spika wa Bunge alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dodoma alisema Profesa Assad amelidhalilisha Bunge kulingana na kauli yake

alisema CAG akiwa nje ya Tanzania wakati anahojiwa na Idhaa ya Kiswahili alisema Bunge la Tanzania kuwa ni dhaifu.

"Kama ni upotoshaji basi CAG na ofisi yake ndiyo wapotoshaji, huwezi kusema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi, na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana," alisema Ndugai.

Ndugai alisema kitendo hicho kimemkasirisha kwani hakutegemea msomi kama huyo angeweza kutoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu uhuru.

Baada ya kuelezea hivyo akamtaka CAG na Halima Mdee kufika mara moja uhojiwa na Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge

Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

CAG alijibu: "Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

"Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa."

Akiendelea kufafanua jibu lake, CAG Assad alisema: "Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua."