Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 12:30 am

NEWS: GABON YAMPIGA MARUFUKU MWANDISHI WA RFI UFARANSA

Mamlaka ya juu ya Mawasiliano nchini Gabon imetangaza jana usiku kwenye runinga kuwa imempiga marufuku mwandishi wa Habari wa Chombo cha Habari cha ufaransa (RFI) Yves-Laurent Goma.

Goma amepigwa marufuku kwa miezi miwili kufanya kazi yake kama mwandishi wa habari nchini humo kuanzia Alhamisi wiki hii.

Hatua hii inakuja kutokana na kwamba mwandishi huyo wa habari aliripoti kwa RFI katika makala yaliyochapishwa Agosti 17 kwamba "Rais wa Gabon Ali Bongo hajawahi kusimama na kusalimia jeshi kama ilivyokuwa wakati wa nyuma." Mamlaka ya Juu ya Mawasiliano imelaani "habari isiyo sahihi ambayo inaonesha picha mbaya na kumkejeli Rais wa Jamhuri Ali Bongo".

Uongozi wa RFI umeelezea masikitiko yake dhidi ya hatua hiyo ya Mamlaka ya Juu ya Mawasiliano nchini Gabon ya kusimamisha kibali cha Yves-Laurent Goma cha kufanyia kazi za uandishi wa habari kwa muda wa miezi mbili.

RFI imebaini kwamba msimamo wake unaendana na uhuru wa habari na inataka mwandishi wake apate kibali cha kufanya kazi haraka iwezekanavyo ili aendelee kutoa habari kuhusu Gabon, kama alivyo kuwa akifanya kwa kipindi chote hicho cha miaka 17.