Rais wa Chama cha wanasheria nchini Tanzania Tanganyika Law Society (TLS) Fatma Karume ameoneshwa kusikitishwa na mfumo wa kimahakama katika utendaji kazi wake kwenye siku za hivi karibuni, hasa utaratibu wa Utoaji haki nchini.
Mwanasheria huyo amesema kuwa Mahakama inapaswa kutekeleza majukumu yake kama yalivyotajwa kwenye Ibara ya 107(A) ya Katiba ya nchi, "inatakiwa kutoa HAKI; kutochelewesha utoaji wa Haki bila ya sababu ya kimsingi na (kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka" amesema Fatma
Akizungumza leo Feb 6, 2019 kupitia hotuba yake aliyoitoa kwa Vyombo vya Habari baada ya kukosa nafasi ya kutoa hotuba kwenye maadhimisho ya siku ya Sheria Duniani yaliyofanyika leo Jiji Dar es salaam ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mh Rais John Magufuli, Bi Karume amesema kusikiliza kesi na kutoa maamuzi ya haki ni vigumu maana inahitaji, KNOWLEDGE, EXPERIENCE, INDEPENDENCE, A SENSE OF DUTY, A CALLING AND FEARLESSNESS. Haki za wananchi si usikilizwaji wa kesi zao tu na haki ya kukata rufaa kwa maana kesi inaweza kusikilizwa, kesi inaweza kukatiwa rufaa bila ya HAKI kutendeka. Kwa mujibu wa katiba yetu majukumu ya Mahakama ni UTOAJI WA HAKI KWA WAKATI.
Hii ni sehemu ya hutuba yake
Tangu utotoni nimefundishwa kwamba vilivyokuwemo kwenye mkoba wa mwanamke ni siri yake. Bibi, Mama au Shangazi akikutuma kumletea mkoba wake, kwetu ilikua marufuku kuchungulia ndani.
Leo, nitaivunja miiko kwa kuwaeleza vichache ninavyobeba kwenye mkoba wangu: miwani, maana sioni vizuri, rangi ya mdomo hii ni muhimu, kipepeo, Dar kuna joto kali, na wanaonijua vizuri wanafahamu ukikuta pesa kwenye Mkoba wangu ni bahati.
Lakini sitoki bila ya kubeba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sitaweza kugawa kila kilichopo ndani ya mkoba isipokua matamshi ya Katiba. Na ningependa kuanza hotuba yangu kwa kuwakumbusha Utangulizi na Misingi ya Katiba yetu. Katiba inaanza na utangulizi ufuatao:
“Kwa kuwa sisi wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu, jamii inayozingatia misingi ya UHURU, HAKI, UDUGU na AMANI: Na kwa kuwa misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo serikali yake husimamiwa na Bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi, na pia yenye Mahakama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa, na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa uaminifu.
“Kwa hiyo basi, Katiba hii imetungwa na Bunge Maalum la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa niaba ya Wananchi, kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya Demokrasia na Ujamaa. “Misingi ya Katiba yetu ni UHURU, HAKI, UDUGU, AMANI, DEMOKRASIA NA UJAMAA.
Ni muhimu pia kutambua kuwa neno Demokrasia limetajwa mara mbili katika utangulizi huu. Na waliotunga Katiba walielewa kwamba Mahakama huru inayotoa haki bila woga wala upendeleo wowote ina hakikisha haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa na ina umuhimu wa pekee kwenye kulinda misingi ya katiba.
Nimeelezwa kwamba uongozi wa Mahakama umeamua kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni : “Utoaji wa Haki kwa Wakati: Wajibu wa Mahakama na Wadau”, na nimeambiwa nijikite kwenye mada hiyo. Nitaanza na Wajibu wa Mahakama na nitamalizia na wajibu wa wadau.
Wajibu wa Mahakama
Wajibu wa Mahakama umewekwa wazi kwenye Katiba yetu. Ibara 107A (1) inasema, “Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utowaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.”
Ibara ya 107A(2)(b) ya Katiba inaeleza, “Katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama zitafuata kanuni zifuatazo, yaani- a) Kutenda haki kwa wote bila ya kujali Hali ya mtu, kijamii au kiuchumi; b) kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi; c) kutoa fidia ipasavyo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine, na kwa mujibu wa sheria mahususi ilioyotungwa na Bunge; d) kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro. e) kutenda haki bila ya kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.”
Ibara 107B “Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi.” Kwa hiyo wajibu wa Mahakama ni kutoa HAKI.
Majukumu ya Mahakama yetu kwa mujibu wa Katiba yetu ni utoaji wa HAKI na si USIKILIZAJI wa kesi tu.
Haki ya kusikilizwa kesi yako ina madhumuni ya kuhakikisha kuwa unapata USAWA MBELE YA SHERIA na si kuhakikisha unapata HAKI mbele ya sheria. Haki inapatikana pale Mahakama itaendeshwa na watu wenye uwezo, uzoefu, weledi, maadili, uhuru wa fikra, ambao hawana uoga na wanaoheshimu matakwa ya Katiba yetu. Kusikiliza kesi na kutoa maumuzi ni rahisi sana, na kila mtu anaweza kufanya hivyo.
Lakini kusikiliza kesi na kutoa maamuzi ya haki ni vigumu maana inahitaji, KNOWLEDGE, EXPERIENCE, INDEPENDENCE, A SENSE OF DUTY, A CALLING AND FEARLESSNESS. Haki za wananchi si usikilizwaji wa kesi zao tu na haki ya kukata rufaa kwa maana kesi inaweza kusikilizwa, kesi inaweza kukatiwa rufaa bila ya HAKI kutendeka. Kwa mujibu wa katiba yetu majukumu ya Mahakama ni UTOAJI WA HAKI KWA WAKATI.
Huwezi ukawa mwoga na hapo hapo ukatoa Haki. Huwezi ukaweka mbele maslahi yako na ukatoa Haki. Utabaki na woga tu lakini Haki (Justice) itakua ndoto. Ili tuelewe umuhimu wa Katiba ningependa kutoa mfano mdogo tu. Kwenye ujenzi wa Standard Gauge Railway, vipimo baina ya vyuma vya reli vitabaki 4ft 8 ½ inch au 1,435 mm kutoka Dar mpaka Rwanda. Hii haiwezi kubadilika hata kama reli inapanda au kushuka mlima. Lakini mabehewa yanaweza kubadilika.
Unaweza kuwa na behewa la kubeba mizigo, behewa la kubeba wanyama, behewa la kubeba mafuta, behewa la kubeba watu daraja la kwanza na behewa la kubeba watu daraja la mwisho ilimradi magurudumu ya mabehewa ni ya kutembea kwenye reli ya standard gauge. Ukiweka behewa lenye magurudumu makubwa au madogo kuliko ya standard gauge, behewa litapinduka na watu watajehuriwa. Ili standard gauge ifanye kazi ipasavyo, lazima magurudumu ya mabehewa yote yafuate muundo wa standard gauge. Kwamba Mahakama lazima ijitathmini yenyewe. Ijiulize mara kwa mara, kweli tunafuata Katiba ipasavyo?
Nisingependa kumaliza bila ya kugusia uendeshaji wa kesi za jinai Tanzania. Sisi Wanasheria tunaona huzuni sana namna criminal justice system inavyotumiwa kuonea na si kuendesha mashitaka dhidi ya watuhumiwa. Watu wanakamatwa na wanawekwa ndani bila ya dhamana wakati upelelezi wa kesi haujakamilika. Nina maswali mawili tu ya kuuliza:
Kama upelelezi haujakamilika unauhakika gani kwamba huyu mtu ana kesi ya kujibu? Kama nitaendelea na mfano wangu wa Standard Gauge, Katiba yetu ya 1977 na mabadiliko yote yaliyofanywa kwenye Katiba hii ni Kama mfumo mpya wa reli. Tujiulize kweli kukamata watu na kuwaweka ndani bila ya haki ya dhamana ni jambo linaloweza kuvumiliwa kwenye mfumo wa Katiba yetu yenye Bill of Rights?
Lingekuwa behewa, hili ni la Standard Gauge au tumeliacha behewa lililoundwa kutembea kwenye reli nyingine litembee kwenye reli yetu na kila likitembea linaathiri wananchi? Tujikumbushe kwamba non-bailable offences zilikuwepo kwa capital offences only hata kabla ya Katiba ya 1977 ninayoifananisha na ujengaji wa Standard Gauge ya Katiba yetu.
Katiba yetu imetambua haki na wajibu muhimu wa wananchi (Bill of Rights), chakusikitisha ni kwamba badala ya makosa yaliyokuwa hayana dhamana kupunguzwa, yanazidi kuongezeka kadri siku zinavyokwenda japokuwa Haki na wajibu Muhimu wa wananchi bado unatambulika na Katiba yetu. Tumefika mahala ambapo makosa ya kutolipa kodi yanakuwa predicate offences kwa makosa ya utakatishaji wa pesa ambayo hayana dhamana. Kwa hiyo mtu akishutumiwa kutokulipa kodi anaweza wekwa ndani bila dhamana kwa kosa la utakatishaji wa pesa.
Na ataswekwa ndani mpaka pale D.P.P atakapoamua kukamilisha upelelezi na kuendelea na kesi. Wakati haya yanatokea, tumesahau kwamba, huyu “mtuhumiwa” ana watoto, ana mke, ana wazazi, ana ndugu na wote wanamtegemea yeye. Siku D.P.P akiamua hataki kuendelea na kesi, “mtuhumiwa” ana i tolewa bila ya fidia. Ninajiuliza kweli hii ni HAKI iliyodhamiriwa na Katiba yetu? Kwa fikra zangu, Hapana, hapana na hapana tena.
Kama nilivyosema awali kazi ya Mahakama ni kuhakikisha Haki inatolewa kwa muda muafaka na kwa kuzingatia misingi ya katiba hasa Haki na Wajibu Muhimu wa wananchi. Tusikae tukamlaumu DPP tu, maana yeye hana wajibu wa kikatiba kutoa HAKI. Wajibu huo ni wa Mahakama.
Kwa hivyo akishitaki watu wakati upelelezi haujakamilika, akifuta mashitaka baada ya mtu kukaa maabusu kwa miaka 6 akaamuru akamatwe tena pale pale Mahakamani, tunaweza kumlaumu kwa kutokufuata maadili ya Waendesha mashtaka, lakini sisi sote kama wananchi, including DPP mwenyewe, tunategemea Mahakama itende HAKI na hakuna muhimili mwingine utakao pata lawama isipokuwa Mahakama maana ibara 107A (1) inasema, “Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utowaji haki katika jamhuri ya muungano itakuwa ni Mahakama”.
Na wajibu huu haukwepeki. Ninakwenda Segerea mara kwa mara na ninataka kuwaambia, December 2018, kulikua na watu walioko gerezani wanaume ni 1,723, kati ya hao waliofungwa kwa mujibu ya hukumu ya Mahakama walikuwa 158 tu na walioko rumande ni 1,565. Upande wa wanawake kulikuwa na walioko gerezani 313, waliofungwa baada ya kesi zao kusikilizwa walikua 66 na walioko rumande ni 247. Hiyo ndio hali halisi ya utoaji wa HAKI kwa upande wa kesi za jinai.
Ningependa kumalizia na ki-joke kimoja, dada yangu mpendwa Balozi Mwanaidi Maajar anapenda kuniambia mara kwa mara. Siku moja Tembo huko Serengeti kamuona Paa anakimbia kweli huku akichungulia nyuma kila baada ya hatua chache. Tembo akamsimamisha Paa akamuuliza “Kulikoni? Mbona unakimbia kama unafukuzwa?” Paa akamjibu huku anahema “Nasikia wanatafuta mbuzi kwa kosa la money laundering”.
Tembo kamtizama Paa kwa mshangao mkubwa akasema “Sasa wewe Paa unakimbia nini? Hujijui kwamba wewe ni Paa sio Mbuzi?” Paa akamtizama Tembo kama vile mjinga kweli akamjibu “Mimi ninajijua kwamba mimi ni Paa, wewe pia unajua kwamba mimi ni Paa, lakini hao wanaotafuta mbuzi wanajua mimi ni Paa? Na kama hawajui itanichukua miaka 20 kuthibitisha mahakamani kuwa mimi ni Paa na Siyani mbuzi. Sina muda huo”.
Alivyomaliza kusema akaendelea kukimbia kama anakimbizwa na ibilisi. Baada ya muda Paa akatizama nyuma akamkuta Tembo naye anakimbia kama anafuatwa na Israeli. Wajibu wa Wadau Sasa ninataka kusema wajibu wa wadau. Ninachukuwa fursa hii kuwakumbusha wananchi wajibu wao ndani ya Ibara ya 26 inayosema kama ifuatavyo:
(1) “Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kuitii Katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano. (2) “Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi”.
Ni wajibu wetu sote kufuata na kuitii Katiba na kuhakikisha hifadhi ya Katiba yetu. Na ni wajibu wetu sote kuilinda Katiba yetu na sheria zetu. Ninataka kumaliza kwa kumnukuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kotoka Hotuba yake “Nyufa” “Hatuwezi kuendelea kupuuza Katiba, ndiyo sheria ya msingi; sheria nyingine zote zinatokana na Katiba.
Haiwezi kupuuzwa na hatuwezi kuendela na uatratibu wa kupuuza Katiba ya nchi yetu au kuwa na Rais anayeonea haya kuitetea Katiba naye amechaguliwa kwa mujibu wa Katiba, ameapa kuilinda Katiba hiyo halafu anona haya hawezi kuitetea Katiba hiyo. Mtu ambaye kawezi kuitetea Katiba ya nchi yetu, hawezi kuilinda, hawezi kuisimamia baada ya kiapo, hatufai. Hafai!”
Ahsanteni.
Fatma Amani Karume President of the Tanganyika Law Society 2018 – 2019 Dar es Salaam, 1st February 2018.