Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 7:07 pm

NEWS: DPP AIOMBA MAHAKAMA KUONGEA NA KABENDERA KUMALIZA KESI

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekubali ombi la Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serekali (DPP) kutaka kukutana na mwandishi wa habari za Kiuchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera kwa ajili ya kukamilisha majadiliano ya kumaliza kesi yake ya Uhujumu Uchumi.

Baada tu ya Ombi hilo Mahakama iliridhia Uamuzi huo leo Jumanne Februari 11, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakamani hiyo, Janeth Mtega baada ya upande mashtaka kuwasilisha ombi hilo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amewasilisha ha ombi hilo na kuiomba mahakama hiyo iruhusu upande wa mashtaka kukutana na mshtakiwa huyo kwa ajili ya kukamilisha majadiliano ya mwisho ya kumaliza kesi hiyo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 17, 2020.

Kabendera anakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha Sh173 milioni.

Januari 27, 2020 kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo, wakili wa Serikali, Gloria Mwenda aliieleza mahakama hiyo kuwa majadiliano kati ya ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka (DPP) na Kabendera yalikuwa yakiendelea.

Kwa mara ya kwanza Kabendera alifikishwa mahakamani hapo Agosti 5, 2019 akikabiliwa na makosa hayo anayodaiwa kuyafanya kati ya Januari 2015 na Julai 2019, jijini Dar es Salaam.

Katika shtaka la kwanza anadaiwa katika kipindi hicho, alijihusisha na mtandao wa uhalifu kwa kutoa msaada kwa genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Shtaka la pili anadaiwa katika kipindi hicho bila ya sababu alikwepa kodi ya Sh173.2 milioni aliyotakiwa kulipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).


Katika shtaka la tatu, anadaiwa kutakatisha Sh173.2 milioni huku akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa la kujihusisha na genge la uhalifu na utakatishaji fedha.