Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 4:34 pm

NEWS: DKT BASHIRU AWAGEUKIA TENA UVCCM

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ameutaka umoja wa vijana UVCCM kuondokana na vitendo vya ukabila, udini, ubaguzi wa rangi, rushwa na kila jambo linalokwenda kinyume na katiba, kanuni na desturi nzuri za nchi, huku akisema vitendo hivyo havina nafasi katika Umoja huo kwa sasa.

Kauli ya Dkt Bashiru aliitoa jana Jijini Dar es salaam wakati akifungua Mkutano Maalumu wa Baraza Kuu la UVCCM taifa.

Pia Dkt Bashiru aliwakumbusha unyeti wa suala la ulinzi na usalama, vijana ndio walinzi wa mwanzo na wananchi kwa ujumla.

“Hivyo uzalendo, nidhamu, kufanya kazi, utii na kujitoa ni misingi muhimu kwa vijana wa CCM,” alisema.

“Jitihada zetu za kujikomboa kiuchumi hazitapokewa vizuri na wasiotutakia mema na maadui walioko ndani na nje ya nchi.

“Kwa mantiki hii, vijana wa ki-Tanzania wana jukumu la kuilinda nchi yetu, kutetea msimamo wetu na kuyasemea mazuri yanayofanywa na Serikali yetu,” alisema.

Kuhusu sayansi na teknolojia, alisema wigo wake ndio ulipo uwanja wa mapambano na ni muhimu kujihami mapema na kuwa tayari kukabiliana mashambulizi ya kimtandao, na wanaotumia mitandao kupotosha kazi nzuri inayofanywa na Serikali lazima wajibiwe kwa hoja na kwa ushahidi wakati wote.