Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 9:28 am

NEWS : DK SHEIN MGENI RASMI MKUTANO WA MBOGAMBOGA

Wakati wakulima wa mbogamboga mjini hapa wakililia soko la uhakika, mkutano wa kimataifa utakaojadili uendelezaji wa kilimo hicho unatarajiwa kuanza kesho.

Mkutano huo unaofanyika mjini Arusha utafunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na utajikita kujadili kilimo cha mbogamboga, matunda na maua.

Meneja Maendeleo wa Chama cha Wakulima wa Mbogamboga (Taha), Anthony Chamanga alisema mkutano huo utajadili masuala ya kuendeleza kilimo hicho ili kuwawezesha wakulima kutambua namna ya kuongeza uzalishaji.


Chamanga alisema wadau wa sekta hiyo watajadili na kukubaliana masuala ya msingi ya kuendeleza sekta ya kilimo ikiwamo namna ya kuwafanya wakulima wazitambue teknolojia mpya zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji. Mkulima wa mbogamboga jijini hapa, Onesmo Peter alisema pamoja na wananchi wengi wakiwamo vijana kuwa na mwitikio katika kilimo hicho wanakabiliwa na matatizo ya upatikanaji wa soko la uhakika na gharama kubwa za pembejeo.

Edward Mollel alisema kilimo hicho kimeshika kasi hususan katika maeneo ya umwagiliaji, lakini changamoto bado ipo katika gharama za uzalishaji tofauti na soko lililopo na kuiomba Serikali kuweka ruzuku katika bidhaa za pembejeo sambamba na kuwatafutia soko la uhakika.