Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 5:27 pm

NEWS: DIWANI ASIMAMISHWA VIKAO 3 KWA KUICHAFUA MANISAPAA MITANDAO YA KIJAMII

Diwani wa Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, Emmanuel Ntobi, amefukuzwa kwenye Baraza la Madiwani na kutohudhuria vikao vitatu vya baraza hilo, pamoja na kunyimwa stahiki zake zote kwa kipindi hicho alichosimamishwa kutokana na tuhuma za kuichafua manispaa hiyo kupitia mitandao ya kijamii.

Imedaiwa diwani huyo mara kwa mara amekuwa akiichafua manispaa hiyo kupitia kwenye mitandao ya kijamii kuwa inafanya ufujaji wa fedha kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo, tuhuma ambazo zimedaiwa siyo za kweli kutokana na kukosekana kwa vielelezo vinavyothibitisha ukweli huo wa matumizi mabaya ya fedha

Naibu Meya wa manispaa hiyo, John Kisandu, alisema wameazimia kumfukuza ndani ya baraza na kutohudhuria vikao vitatu mfululizo na kukosa stahiki zake zote.

Alisema kwa mujibu wa kanuni za kudumu za halmashauri, mjumbe ambaye atatoa kashfa za kuichafua manispaa na kushindwa kuthibitisha ukweli, achachukuliwa hatua kwa kusimamishwa kuhudhuria vikao vitatu pamoja na kukosa stahiki zake zote ikiwamo posho, nauli na kinga ya matibabu.

"Kanuni ya 28 kipengele cha tatu za kanuni za kuduma za halmashauri (2013) namba mbili, kinasema endapo mjumbe aliyetoa hoja za kashfa akakataa kufuta kauli yake kwa kuomba msamaha kwa maandishi kama alivyoelekezwa na kamati ndogo, meya wa mkutano atamsimamisha mjumbe huyo kuhudhuria vikao vitatu na kunyimwa stahiki zake zote," alisema Kisandu.

Kwa upande wake diwani huyo, Emmanueli Ntobi, alikiri tuhuma ambazo amekuwa akizotoa ni za kweli kuwa manispaa hiyo ya Shinyanga inafanya ufujaji wa fedha kwenye utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo, na kubainisha maamuzi yaliyotolewa hakubaliani nayo bali atakwenda kudai haki yake mahakamani.

Aidha, alisema anaiomba serikali kuu iunde tume ya kwenda kuichunguza miradi ya maendeleo ya manispaa ya Shinyanga ambayo inatekelezwa kama haifanyi ufujaji wa fedha, ukiwamo mradi wa machinjio ya kisasa, upimaji wa viwanja pamoja na ujenzi wa kituo cha afya Kambarage.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Boniphace Chambi, aliwataka madiwani wa manispaa hiyo kuacha kuitumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuichafua serikali na kama wanahoja waziseme kwenye vikao vyao vya baraza na zisipo shughulikiwa waende kwenye mamlaka zingine ikiwamo Takukuru.