Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 1:30 pm

NEWS: DEREVA TAKSI KIZIMBANI AKITUHUMIWA KUMTEKA MO DEWJI

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam limemfikisha katika Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu Dereva Teksi Mousa Twaleb (46), akishtakiwa kwa makosa matatu likiwemo kosa la kuhusika kumteka mfanyabiashara na Bilionea Mohamed Dewji Maarufu kama MO tukio lilitokea Oktoba 11, 2018 Jijini Dar es salaam.

Twaleb amepanda kizimbani leo saa nne asubuhi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Akisomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali Simon Wankyo, mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Mei Mosi mwaka 2018 na Oktoba mwaka huo jijini Dar es Salaam na Johannesburg, nchini Afrika Kusini.

Mo alitekwa na watu wasiojulikana alfajiri ya Oktoba 11, 2018 wakati akifanya mazoezi katika Hoteli ya Colosseum iliyopo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, alipatikana Oktoba 20 katika eneo la Gymkhana baada ya kudaiwa kutelekezwa na watekaji hao.

Kadushi amedai mshtakiwa alijihusisha na genge la uhalifu, walimteka Mo katika Hoteli ya Colleseum iliyopo wilayani Kinondoni na kumficha.

Mshtakiwa huyo pia anadaiwa kutakatisha Sh milioni nane ambazo alijipatia huku akijua zinatokana na mazalia ya kosa la uhalifu.

Mshtakiwa huyo hakutakiwa kujibu lolote sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Kesi imeahirishwa hadi Juni 11, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Watu 12 walikamatwa na polisi katika tukio hilo wakihusishwa na watekaji. Familia ya Dewji iliahidi kutoa Sh1 bilioni kwa mtu yeyote ambaye angetoa taarifa ambazo zingesaidia kupatikana kwa kijana wao. Hata hivyo hakuna aliyepata fedha hizo baada ya kupatikana kwake.

wamujibu wa jarida la masuala ya fedha la Forbes, MO ndiye tajiri namba moja Afrika Mashariki, na tajiri mdogo zaidi Afrika akiwa na ukwasi wa dola bilioni 1.5.

Kampuni yake ya METL, ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.

Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.

Bilionea Mohammed DewjiHaki miliki ya pichaAFP/GETTY

Kwa mujibu wa tovuti yake, METL inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na petroli na utengenezaji baiskeli.

Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.

Inaendesha shughuli zake Tanzania, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Malawi, Msumbiji na Zambia, ambapo huajiri moja kwa moja watu zaidi ya 28,000.

Shughuli za MeTL huchagia 3.5% ya jumla ya pato la taifa (GDP) la Tanzania.

Kiwango cha wastani cha ukuaji wa mapato ya kampuni hiyo kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2014 kutoka $30 milioni hadi $1.3 bilioni kilikuwa ni 200%.