Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 5:24 pm

NEWS: DC SHEKIMWERI AMEWATAKA WACHIMBAJI WADOGO KUWA WAZALENDO.

MPWAPWA: Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri amewataka wachimbaji wadogo kutambua na kuenzi azma ya Rais dokta John Magufuli kwa kuwa wazalendo kwenye kulipa kodi na tozo mbalimbali stahiki ikiwemo na kuwafichua waotorosha madini.


Agizo hilo amelitoa wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wadogo akiwa ziarani katika mgodi wa machimbo ya dhahabu katika Kijiji cha Kikuyu kilichopo katika kata ya Ipera wilayani humo.

Amesema Rais Magufuli alishaongea na wachimbaji hao na kuwaeleza azma yake njema katika kuhakikisha madini yananufaisha nchi.


“Mkilitekeleza hilo mtakuwa mmemuunga mkono Rais wetu anayepambana kuhakikisha rasilimali za nchi yetu zinalindwa,hivyo sisi tulio chini yake tusimwangushe,”alisema Shekimweri.

Amesema serikali inatambua wanachofanya na inawathamini na ndio maana ameona umuhimu wa kuwatembelea na kufahamu kazi zao.

“Ndugu zangu wachimbaji wadogo,eleweni kuwa serikali yenu ya wilaya ipo tayari kuona mkiendelea na shughuli zenu za uchimbaji mradi tu mzingatie Sheria, Kanuni na Taratibu za Tasnia ya Madini kikamilifu,”alisisitiza mkuu huyo.


Katika kufanya shughuli zao hizo amewahimiza kuhifadhi mazingira kwa kuwa uchimbaji wa madini holela huchochea ukataji wa miti hivyo,kujiepusha na uvunjifu wa amani,uhalifu,matumizi ya dawa za kulevya na vilipuzi.

Katika ziara yake hiyo amebaini uwepo wa ajira za watoto chini ya umri wa miaka 18, kukosekana kwa vyoo,kuwepo ukataji miti na ufinyu wa huduma hususani maji safi na Salama.

“Watoto hawa wanatakiwa kuwa shule,umri wao hauruhusu kujishughulisha na shughuli hizi,hizi ni ajira kwa watoto ambazo serikali yetu inapigia kelele,niwaagize wazazi na walezi hakikisheni watoto wanaenda shule na sio kuwepo mahala hapa,”aliagiza Shekimweri.

Amekemea kitendo cha wanunuzi walioanza kufanya Biashara kwenye soko kubwa la Dar es Salaam na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanunuzi na wauzaji hao wana kwenda kuripoti kwake na risiti walizouzia ili kodi (ya ushuru wa huduma) iweze kukokotolewa.

Shekimweri akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji na Wataalamu kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mfawidhi Mkoa wa Dodoma,ametoa nafasi kwa wataalamu wote kutoa elimu kuhusu masuala mtambuka ya uchimbaji salama pamoja na tamko ya sera za madini.

Amesema wilaya inakamilisha taratibu za uanzishwaji wa soko la Madini Wilaya na linatarajiwa kuanza rasmi Oktoba Mosi 2019.

Wakati wakihitimisha, wachimbaji wameomba siku saba kufanyia kazi mapungufu yote ambapo Mkuu huyo wa wilaya aliridhia ombi hilo na kuwataka washirikiane na wataalamu kwa maelekezo na miongozo itekelezwe kwa ufanisi ikiwemo kuunda uongozi, kushughulikia usajili, kuandaa idadi ya wachimbaji na kujenga vyoo.

Pia ameiagiza Ofisi ya Madini Mkoa, kuratibu ushauri wa kitaalamu na upatikanaji wa Mitambo rafiki ya mazingira kupitia Wakala wa Giolojia Tanzania(GST) na Stamico.