Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 12:15 pm

NEWS: DC AWATAKA WANANCHI KUACHA KUKATA MITI OVYO.

BAHI: Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma, Mwanahamisi Munkunda, amewataka wananchi kuacha kukata miti ovyo ili kulinda uoto wa asili,pia amewaagiza wenyeviti wa vijiji kuhakikisha hakuna miti inayokatwa katika maeneo wanayoyasimamia.

Pia amelipongeza Shirika la Lead Foundation, kupitia mradi wake wa kisiki hai kwa namna linavyosaidia katika kurudisha uoto wa asili kwa kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutunza visiki na kuchipua upya kurudi katika hali yake.

Mkuu huyo ametoa maagizo hayo katika kijiji cha Mpamantwa Wilayani humo, wakati wa uzinduzi wa vipindi vya kisiki hai katika radio mbalimbali ambavyo vitasaidia kutoa elimu kwa jamii namna ya kutunza visiki kwa njia ya radio katika maeneo yaliyoathiriwa na ukataji miti, ili kusaidia kurudi katika hali yake, tukio lililoenda sambamba na ugawaji zawadi kwa vinara wa kusitawisha miti kwa njia ya kisiki hai.

Amesema kila mtu katika eneo lake ahakikishe analinda mazingira kwa kuepuka kukata miti ovyo kwani uoto wa asili huo ukipotea kuurudisha ni kazi kubwa, na ulimwenguni kote wanatumia gharama kubwa katika kurudisha uoto wa asili.

"Wazo la kisiki hai ni wazo lenye manufaa makubwa Sana kwani hata siku akiondoka misitu itakayokuwepo itakuwa ni alama kubwa sana ambayo atakuwa ametuachia kazi itabaki kwetu kuiendeleza, maana uliamua kurudisha uhai wetu sisi na viumbe vingine ambavyo vilikuwa vinapotea kwa kuharibu uoto wa asili"

"Sisi tumeshazuia uvunaji wa mti wowote hata Kama ni wakwako huwezi kuvuna mpaka kibali hata Kama unaandaa shamba ni marufuku kukata mpaka upate kibali, na maeneo yote yanayomilikiwa na serikali ya kijiji ndio yawe mfano" amesema DC Mwanahamisi.

Amesema moja ya miradi anayoipenda na kuifurahia ni huo wa kisiki hai, kwa ni wamatokeo ya haraka na pia unasaidia na kuokoa maisha ya viumbe wengine wanaotegemea mazingira kwa sababu kwa mda mfupi wameweza kurudisha uoto katika eneo walilolitenga.

"Huu mradi naupenda na ninaufuatilia ni wa kisiki hai kwa sababu ni wa mda mfupi wa mwaka mmoja kuna eneo tulitenga kwa mda mfupi tayari umekuwa msitu na uoto wa asili umeweza kurudi na tumetunza mazingira" amesema.

Amepongeza uongozi wa kijiji Cha Mpamantwa kwa kuchagua baadhi ya milima na kuihifadhi Kama mfano na kuzuia shughuri zozote kufanyika katika eneo hilo na kufanya kuwa mfano ili wananchi waweze kuiga mfano huo.

Amesema kuwa ukataji ovyo wa miti unatishia kupotea kwa viumbe vingi na kupoteza uoto wa asili, ametolea mfano wa kijiji hicho kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na kilimo Cha miwa na nyanya kwa mwaka mzima lakini kutokana na uhalibifu wa mazingira shughuli hizo kwa Sasa hazifanyiki kwa ardhi kupoteza uoto wake wa asili.

Kwa upande wake Meneja Program mradi wa kisiki hai, unaoendeshwa na Shirika la Lead Foundation, Njamasi Chiwanga, amesema mradi huo ulianzishwa mwaka 2018, unatekelezwa katika Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma,na vijiji mia tatu vimeweza kunufaika katika mradi huo na kufanyika kwa mafanikio makubwa Sana.

Amesema mradi huo umekuwa na mafanikio kwa sababu wanatumia wanakijiji ambao wamewapa mafunzo na kuwaita machampioni, na wao kwenda kuwafundisha wananchi wengine katika maeneo wanayotoka.

Amesema tangu mradi huo kuanzishwa wameotesha miti zaidi ya milioni nne katika Mkoa mzima wa Dodoma

Mradi huo wa Elimu kisiki hai radioni unaendeshwa na shirika la Lead Foundation, kwa kushirikiana na mashirika wenza ambayo ni Jast digiti, Farm radio international na Radio Dodoma fm kwa Mkoa wa Dodoma.