Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 1:13 am

NEWS: CUF MAALIM SEIF YAIOMBA MAHAKAMA KUHARAKISHA HUKUMU YA LIPUMBA

Dar es Salaam: Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Shariff Hammad kimeiomba Mahakama kutoa hukumu ya shauri namba 23/2016 linalohoji uhalali wa uwepo wa nafasi ya Uwenyekiti kwa Profesa Ibrahim Lipumba katika chama hicho.

Hayo yamezungumzo leo Jumanne Februari 26, 2019 na wabunge wawili wanao muunga mkono Katibu mkuu wa chama hicho, Ally Saleh (Malindi) na Hamidu Bobali wa Mchinga wakati wakizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wabunge wa chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam.

Saleh amesema kuwa ucheleweshwaji wa hukumu ya shauri hilo unawasababishia madhara ikiwamo kuibiwa fedha za ruzuku zaidi ya Sh1.5 bilioni, kuondolewa kwenye nafasi za uongozi na kuwapo kwa mashauri mengi mahakamani yanayowagharimu fedha na muda.

Saleh ambaye ni mnadhimu wa kambi ya CUF bungeni amesema si lengo lao kutoa shinikizo la aina yoyote, kuingilia taratibu za mahakama ila wanaomba shauri hilo litolewe hukumu. "Tupo tayari kwa hukumu yoyote itakayotolewa, ila tumepata mashaka namna shauri hilo linavyoahirishwa mara kwa mara licha ya kuwa limeshasikilizwa," amesema Saleh

"Kwa heshima na taadhima tunamuomba Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi waliangalie suala hili kwa umuhimu na uzito maalumu kwa sababu kuchelewa kwake kunakiathiri chama chetu kwa kiasi kikubwa," amesema.

"Tunashindwa kufanya siasa, kwa sababu baadhi ya maeneo wenyeviti wa chama kwa eneo husika wanakuwa upande wa Lipumba na sisi tupo upande halali wa Maalim Seif, huu mkanganyiko unatusukuma kuiomba mahakama kutoa hukumu ya kesi hiyo ili tuendelee na majukumu yetu angalau kwa kipindi hiki kifupi kabla ya uchaguzi mkuu 2020," amelalama Bobali.