Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 10:57 pm

NEWS: CHMTs KAGERA WAFUNDWA KUJIKINGA DHIDI YA UGONJWA WA EBOLA

KAGERA: Timu za uendeshaji huduma za Afya za Halmashauri (CHMTs) za Mkoa wa Kagera zimeelekezwa jinsi ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Ebola, ikiwa ni moja kati ya mikakati ya Serikali kuwakinga Watumishi wa Sekta ya Afya endapo utaingia nchini.

Hayo yamejiri wakati wa mafunzo juu ya njia bora ya namna ya kujikinga na kudhibiti magonjwa (Maambukizi) kwa kuzingatia taratibu za utoaji huduma kwa mgonjwa (IPC Standard) inayoendelea Mkoani Kagera ikiwa ni moja kati ya mikoa iliyo katika hatari ya kupata ugonjwa wa Ebola.

Katika Mafunzo hayo, Afisa kutoka Kitengo cha Dharura na Maafa Wizara ya Afya Dkt. Alex Sanga amesema kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo zipo katika hatari ya kupata wagonjwa wa Ebola kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu na ukaribu na Nchi ya Uganda na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo ambazo tayari zimekwishapata janga hilo.

Dkt. Sanga amesema kuwa, taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema kuwa takribani zaidi ya Wagonjwa 2950 wamethibitika kuwa na Ugonjwa wa Ebola, huku zaidi ya Wagonjwa 2000 wakipoteza maisha tokea mlipuko huo ulipojitokeza Agosti 2018, huku Wataalamu wa Afya 131 walipata maambukizi, ambapo 41 kati yao wamepoteza maisha.

Aidha, Sanga amesema kuwa Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utayari wa kukabiliana na tishio la Ugonjwa huo ili kuhakikisha hauingii nchini, ikiwemo kuelimisha jamii njia za kujikinga na Ugonjwa ili kuzuia usiingie nchini, na kutoa Elimu kwa Watoa huduma za Afya juu ya kumuhudumia mtu mwenye dalili za Ebola endapo atatokea.

"Watoa huduma wanatakiwa kuzingatia taratibu za kujikinga na kudhibiti maambukizi (IPC Standard precautions) kwa kadri Miongozo inavyoelekeza wakati wote watoapo huduma kwa Wagonjwa, jambo litalosaidia kuwaepusha kupata maambukizi, au kumsaidia mgonjwa kupata maambukizi mapya wakati wa matibabu” Alisema Dkt. Alex Sanga.

Hata hivyo, Dkt. Sanga amesema kuwa, Shirika la Afya Duniani (WHO) inakusudia kuzuia Ugonjwa wa Ebola kwa kuimarisha huduma za uchunguzi na kusaidia nchi zilizo katika hatari ya kupata ugonjwa wa Ebola.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Maabara kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi MUHAS Akili Mawazo Mwakabhana amesisitiza umuhimu wa kufuata taratibu na miongozo wakati wa kutoa huduma kwa mgonjwa kuzuia maambukizi mapya kwa Mgonjwa au Mtoa huduma za Afya jambo ambalo litasaidia kupunguza idadi ya Wagonjwa na kuokoa fedha ambazo zingetumika katika matibabu.

Aliendelea kusisitiza kwa kutoa wito kwa watoa huduma za Afya kuacha kufanya kazi kwa mazoea hali itakayosaidia kuondoa tatizo la usugu wa magonjwa (Wadudu) kutokana na matumizi mara kwa mara ya dawa, ambayo daktari angeweza kuyazuia kwa kufuata miongozo wakati wakutibu ugonjwa.