Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 4:44 am

NEWS: CHANJO KUZUIA UGONJWA WA MAPAFU YA NG’OMBE YAINGIA SOKONI, YA KICHAA CHA MBWA MBIONI KUZALISHWA NCHINI.

SIMIYU: Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa wito kwa wananchi hususan wafugaji kuchanja ng’ombe wao dhidi ya ugonjwa wa mapafu ya ng’ombe (CBPP) ambao husababisha vifo kwa mifugo hiyo.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mifugo nchini Dkt. Hezron Nonga akizungumza katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nanenane) kwenye viwanja vya Nyakabindi katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu amesema chanjo hiyo iliyoanza kutumika nchini Mwezi Julai mwaka huu inapatikana kwa Shilingi 200 hadi 250 pekee.

“Ugonjwa wa mapafu ya ng’ombe unasababisha kifo usipomkinga ng’ombe wako kwa kutumia chanjo hii utaingia gharama kubwa kwa kuwa ng’ombe huyo atakufa pia utatumia gharama kubwa kuwalinda ng’ombe wengine ulionao.” Amesema Dkt. Nonga

Akizungumzia zaidi kuhusu chanjo hiyo Dkt. Nonga amesema chanjo tayari ipo sokoni nchi nzima na kwamba vipo vituo 11 kila kanda na inapatikana kwa Shilingi 200 hadi 250 pekee na kuwataka wafugaji kuhakikisha ng’ombe wanachanjwa dhidi ya ugonjwa huo.

Aidha amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Kituo cha Kuzalisha Chanjo Kibaha (TVI) kilichopo Mkoani Pwani inatarajia katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili kuanza kuzalisha chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa ambazo kwa sasa zinanunuliwa kutoka nchi za nje.

Kutokana na watu wengi kuwa na utaratibu wa kumiliki mbwa katika makazi yao katika kipindi cha siku za hivi karibuni, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Mifugo nchini Dkt. Hezron Nonga amewataka watu wanaomiliki mbwa kuhakikisha wanyama hao wanachanjwa kwa kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa hauna tiba endapo binadamu atang’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huo.

“Tunataka hii chanjo iwe inapatikana kila mahali pamoja na kufanya msako nchi nzima kwa watu wanaomiliki mbwa lakini hawapeleki mbwa hao kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.” Amesema Dkt. Nonga

Amefafanua kuwa kwa kawaida chanjo hiyo hupatiwa mbwa mara moja kwa mwaka ambapo kwa sasa inapatikana kwa Shilingi Elfu Moja pekee ili kuhakikisha wamiliki wa mbwa na wananchi wanakuwa salama.