Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 12:33 am

NEWS: CHAMA CHA WAZARI MKUU WA UINGEREZA CHAPOTEZA VITI VINGI BUNGENI

London: Chama cha Conservative cha Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May kimepoteza wingi wa viti bungeni baada ya uchaguzi wa Alhamis ulioitishwa mapema na May kuelekea mazungumzo ya Brexit ya kujiondoa Umoja wa Ulaya.

Wapigakura nchini Uingereza wamempiga dafrau kubwa waziri mkuu wao kwa kumkosesha ushindi wa moja kwa moja kuweza kuunda serikali ya chama chake cha Conservative.

Hata hivyo, kwa kuwa hakuna mshindi wa wazi wa uchaguzi huo wa jana (Juni 8), May ameashiria kwamba huenda akabakia kwenye nafasi yake ya uwaziri mkuu, akiongoza serikali isiyokuwa na wingi wa kutosha bungeni.

Mpinzani wake, Jeremy Corbyn wa chama cha Labour, amemtaka May ajiuzulu na ampishe kuunda serikali. Wachambuzi wa mambo wanasema uamuzi wa May kuitisha uchaguzi wa mapema, zaidi ya miaka miwili kabla ya wakati, lilikuwa kosa, na pia kampeni zake zilikuwa na mapungufu makubwa.

Kati ya viti 647 kwenye 650 vilivyotangazwa, Conservative imejikingia viti 316, pungufu ya viti kumi kuweza kuunda serikali yenye wingi bungeni. Labour kimepata viti 261.