Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 5:36 am

NEWS: CHADEMA YAMSHTAKI RAIS WA TFF WALLACE KARIA

Dar es Salaam: Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania kimeandika barua kwenda kwa Rais wa Shirikisho la mpira wa miguu Duniani (Fifa), Gianni Infantino likimshtaki Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia kwa kutoa kauli za kibaguzi na unyanyasaji dhidi ya viongozi wa Kisiasa nchini Tanzania.

Katika barua hiyo ya kurasa mbili, iliyosainiwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumain Makene imeonyesha masikitiko yake kwa kitendo cha Karia kutumia mchezo wa soka kuonyesha chuki na ubaguzi dhidi ya Tundu Lissu ambaye Septemba 7, 2017 alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 jijini Dodoma.

"Tunaandika barua hii kuelezea masikitiko yetu na kupinga kauli iliyotolewa na Rais wa TFF, Wallace Karia ambayo inaunga mkono uvunjaji wa haki za binadamu, uhuru wa kuzungumza na kuchochea ubaguzi wa kisiasa jambo ambalo ni kinyume na miiko ya mchezo wa mpira wa miguu unaosimamiwa na Fifa," imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo ambayo pia imeelekezwa kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na Karia mwenyewe, imeambatanishwa pia na ushahidi wa kipande cha video kinachomuonyesha Rais huyo wa TFF akitoa kauli hiyo.

Jumamosi ya Februari 2, 2019 jijini Arusha katika mkutano mkuu wa TFF, Karia alikemea watu wenye tabia alizoziita za ‘u Tundu Lissu’ katika soka, kamwe hawezi kukubali kuona wakiendelea kukosoa uongozi wa TFF.

Baada ya mkutano huo Karia alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu kauli hiyo alisema, “Nimesema kama kuna ‘ma Tundu Lissu’ kwenye mpira, nadhani mnaelewa Lissu anahangaika kwenye vyombo vya habari kuikashifu Serikali na (Michael) Wambura anazungumza kwenye vyombo vya habari kuikashifu TFF na uongozi wa TFF.”

Katika ufafanuzi huo Karia pia alisema kama kuna watu amewakwaza kwa kauli hiyo anawaomba msamaha.