Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 9:40 am

NEWS: BUNGE LAISHA MAJALIWA ASISITIZA MAMBO 12 MAZITO

DODOMA: WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge la Bajeti kwa kuainisha mambo 12 mazito, aliyosisitiza kwa wananchi huku akieleza kuwa hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari. Lakini, ameonya kuwa serikali itahakikisha waliohusika na mauaji yanayotokea mkoani Pwani, wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki.

Waziri Mkuu alisema hayo mjini hapa jana wakati akiahirisha mkutano huo, ambapo alizungumzia masuala la Hali ya Ulinzi na Usalama, Uratibu wa Maafa, Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2017/18, Sekta ya Kilimo (hasa hali ya chakula na pembejeo), sekta za Ardhi, Wanyamapori, Afya, Elimu, Maji, Uboreshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini, Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya na Michezo.

Akizungumzia hali ya usalama nchini, alisema kwa ujumla hali ya ulinzi na usalama nchini ni shwari huku akiwaonya wale wanaofanya viashiria vya kiuhalifu kuwa watasakwa kwa nguvu zote. Alisema, “Usalama wa raia na mali zao unaendelea kulindwa, na mipaka yote ya nchi yetu iko salama, vikosi vya ulinzi na usalama viko imara na madhubuti katika kulinda mipaka na usalama wa nchi yetu.”

Mauaji Kibiti Alisema pamoja na nchi kuwa shwari, wapo baadhi ya watu wanaotishia usalama kwa kushiriki kwenye vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha, akitolea mfano matukio ya hivi karibuni ambapo kumekuwapo na mauaji ya kuvizia katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani.

Alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa kila raia wa Tanzania, wakiwemo wananchi wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji wanakuwa huru kufanya shughuli zao za maendeleo bila kuhofia usalama wa maisha yao.

“Serikali inaendelea kuchukua hatua za muda mfupi na za muda mrefu ili kurejesha hali ya usalama katika maeneo hayo. Tumeongeza doria na vitendea kazi kwa askari. Pia tumefanya maamuzi ya kuunda Kanda Maalum ya Kipolisi.

Mauaji ya Wananchi wetu na askari wetu hayakubaliki na wala hayavumiliki, kwani askari ndio walinzi wetu sisi pamoja na mali zetu,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza: “Tishio kwa walinzi wa amani na wananchi wetu ni tishio kwetu sote, hivyo serikali itahakikisha waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki. Wanaweza kukimbia, lakini hawataweza kujificha daima.

Tutawakamata!” Aliongeza kuwa “Tumeanzisha mfumo wa kuhakiki nyaraka, hususan vibali vya kuishi nchini pamoja na Hati za Kusafiria na kuhuisha utaratibu wa kisheria wa kutoa hati kwa wahamiaji walowezi, ili kuweza kuwatambua kwa urahisi. Kwa jitihada hizi, tutaweza kudhibiti nyaraka za kughushi na kudhibiti wahalifu wa kimataifa wanaovuka mipaka.”

Kuhusu Uratibu wa Maafa, alisema serikali inakamilisha mifumo ya ufuatiliaji wa maafa kwenye Kituo cha Uratibu na Mawasiliano wakati wa Dharura, kuainisha na kutambua maeneo hatarishi kwa maafa pamoja na kuendelea kuijengea uwezo Idara yetu ya Uratibu wa Maafa.

Hali ya chakula nchini Majaliwa alisema hali ya chakula siyo ya kuridhisha sana, kwani bado kuna maeneo yenye upungufu wa chakula, na kwamba ili kukabiliana na upungufu huo, serikali ilifikia uamuzi wa kupiga marufuku usafirishaji mahindi nje ya nchi bila kibali, badala yake tunahamasisha uongezaji wa thamani ya mazao badala ya kusafirisha nafaka ghafi.

“Nashauri wafanyabiashara wasambaze mahindi kwenye maeneo ambayo hayana chakula cha kutosha ndani ya nchi kuliko kupeleka nje ya nchi,” alieleza na kutoa mwito kwa wakuu wa mikoa ya mipakani kutekeleza agizo la serikali la kuchukua hatua kwa watakaokiuka agizo hilo.

Kuhusu mfumo wa usambazaji wa mbolea, alisema serikali imeamua kuimarisha utaratibu wa upatikanaji na usambazaji mbolea kupitia Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja, ambayo itaagizwa na waagizaji watakaopitishwa kupitia zabuni, na wakulima watanunua katika maduka ya pembejeo vijijini kwa bei dira itakayopangwa na serikali. Mimba shuleni Alisema vita ya kupambana na mimba kwa wanafunzi si ya mtu mmoja, bali ipo kisheria.

“Kuwaachisha masomo wanafunzi waliopata ujauzito, ni utekelezaji wa Waraka na Kanuni za Elimu za Mwaka 2002 zinazohusu kufukuza na kuondoa wanafunzi shuleni kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo uasherati, wizi, ulevi, kutumia dawa za kulevya pamoja na utoro unaotokana na baadhi ya wanafunzi kwenda kufanya shughuli za biashara ndogo ndogo, kucheza kamali, kuvua samaki, kuchimba madini,” alieleza.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, jumla ya wanafunzi 3,637 waliacha masomo kutokana na kupata ujauzito. Alisema msimamo wa serikali wa kutoruhusu wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo katika mfumo rasmi wa elimu ni kwa mujibu wa sheria na wala sio utaratibu mpya kama inavyopotoshwa na baadhi ya wanaharakati.

“Msimamo huo wa kisheria unalenga kuwafanya watoto wa kike wajishughulishe na masomo yao badala ya kushiriki kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili. Lengo hili lina nia ya kuwahimiza wazazi wawafundishe watoto wao mambo mema,” alifafanua.

Hivi karibuni, Rais John Magufuli alipiga marufuku wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea na masomo na kuwataka wale wanashabikia hilo wanaanzisha shule zao. Serikali za Mitaa Katika juhudi za kuimarisha utendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Majaliwa alitoa mwito kwa viongozi wa mikoa na wilaya pamoja na halmashauri, kuhakikisha malalamiko yote ya wananchi yanatatuliwa haraka katika ngazi husika.

Dawa za Kulevya Kuhusu dawa za kulevya, alisema azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kutokomeza mtandao wa dawa za kulevya nchini kwa kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanakuwa endelevu, yanafanyika kisayansi na yanaleta mafanikio na kuutaka umma kuunga mkono mapambano hayo.

Ardhi, Afya Aidha, alisema serikali imeweka Mkakati na Mpango Kazi wa kuwezesha kufikia lengo la kupanga matumizi bora ya ardhi katika vijiji 1,500 na wilaya tano kila mwaka. Alisema serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki za kupunguza gharama za umilikaji wa ardhi.

“Katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, serikali imepunguza tozo ya mbele kutoka asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi hadi asilimia 2.5 tu. Natoa wito kwa wananchi kuchangamkia punguzo hili na kujitokeza kupimiwa na kumilikishwa ardhi,” alieleza.

Katika afya, aliwahakikishia wanawake wote nchini kwamba hakuna mwanamke mjamzito atakayepoteza maisha kwa kukosa dawa, sindano ya kuzuia kuvuja damu au kukosa dawa ya kuzuia kifafa cha mimba.

Alisema serikali imeamua kwamba itanunua, kusambaza na kutoa bila malipo dawa kwa ajili ya uzazi salama katika vituo vya umma vya kutolea huduma, hii ni pamoja na dawa ya kuzuia kutokwa na damu baada ya kujifungua, dawa kwa ajili ya kifafa cha mimba na dawa kwa ajili ya kuongeza damu.

Sh bilioni saba zimetengwa kwa kazi hiyo. Bajeti ya Serikali 2017/18 Alieleza kuwa kura za wabunge kupitisha Bajeti ya Mwaka 2017/2018 ni kielelezo kwamba bajeti hiyo inajibu kiu ya wananchi ambao wabunge wanawakilisha.

Sekta ya wanyamapori Alisema kutokana na kuwepo kwa migogoro baina ya wafugaji na wakulima na migogoro baina ya wafugaji na wahifadhi wa mapori, ameelekeza kwamba ifikapo mwisho wa mwezi huu, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wabainishe maeneo yote ya Ranchi za Taifa za Mifugo ambazo hazitumiki na kuzigawa katika vitalu (blocks) kwa wafugaji ili mifugo mingi iondolewe vijijini na ipelekwe kwenye maeneo hayo ili serikali itoe huduma za ugani za kisasa kwenye vitalu hivyo.


source: habari leo