Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 7:54 am

NEWS: BODABODA WATAJWA KUNYANYASA WASICHANA KIMAPENZI

DAR ES SALAAM: WAFANYABIASHARA ya huduma za usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda, wametajwa katika utafiti kuwa wanaowanyanyasa kimapenzi na kuwafanyia ukatili wasichana wanaokataa kushirikiana nao kimapenzi.

Kwa mujibu wa matokeo ya Utafiti uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Maadili Center na kutolewa jana na Mwenyekiti wa shirika hilo Florentine Senya, watoto wengi wa kike walitaja kero kubwa kuwa ni waendesha pikipiki hao (bodaboda) kuwanyanyasa hadi kufikia hatua ya kutishia kuwagonga kwa pikipiki zao wasichana hao wanapokataa kujihusisha nao kimapenzi.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu utafiti wa malezi na maadili ya watoto wa kike uliofanywa na shirika hilo, Senya alisema utafiti huo unaendelea hadi sasa ulifanywa katika shule za sekondari na msingi kwa mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, utafiti huo pia umebaini kuwa asilimia 78 ya familia nyingi zina matatizo ikiwemo wazazi kutelekeza familia zao na kuwaacha wengi kujihudumia wenyewe jambo linalochangia kuwapo ongezeko la watoto wasio na maadili.

Alisema utafiti umebaini kuwa, watoto wa kike 10 kati ya 50 sawa na asilimia 20, wamepitia vitendo mbalimbali vya ukatili ikiwemo kupigwa na wazazi, kuchomwa moto wanapokosea, na hata kutishiwa maisha wanapokataa kujihusisha kimapenzi na watu waliowazidi umri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Maadili Center, Rosaline Castillo alitaka jamii ikubali ukweli kuwa wazazi wengi wametelekeza watoto katika malezi.

SOURCE: HABARI LEO