Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 9:53 am

NEWS: BILIONEA DANGOTEA AMTAHADHARISHA RAIS MAGUFULI


Dar es Salaam. Bilionea namba moja barani Afrika, Aliko Dangote amemtahadharisha Rais John Magufuli kuwa vitendo vyake vinaogofya na kukimbiza wawekezaji.

Raia huyo wa Nigeria ameyasema hayo ikiwa ni miezi sita tangu alipopewa sehemu ya mgodi wa makaa ya mawe uliopo Ngaka mkoani Ruvuma ili achimbe yatakayotosheleza kuendesha kiwanda chake cha saruji kilichopo mjini Mtwara.

Dangote amelaumu sera za Serikali akisema, “zinawatisha wawekezaji wengi. Kuwatisha wawekezaji si kitu kizuri. Mmoja akitishwa wengine watakimbia bila hata kuhitaji maelezo.”

Tajiri huyo amesema hayo na kunukuliwa na gazeti ya Financial Times la Uingereza.

Dangote ametoa maoni hayo binafsi akiwa nchini Uingereza anakohudhuria kongamano la wawekezaji wa Afrika lililoandaliwa na gazeti hilo maarufu kama Financial Times Africa Summit linalofanyika jijini London.

Malalamiko ya Dangote yanatokana na sheria mpya ya usimamizi wa rasilimali za Taifa iliyopitishwa Julai inayopendekeza Serikali kuwa na walau asilimia 16 kwenye miradi yote iliyowekezwa kwenye sekta ya madini.

Hata hivyo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alipoulizwa kuhusu hoja ya Dangote alisema ana wasiwasi kama mfanyabiashara huyo anaweza kusema hivyo kutokana na jinsi Serikali inavyomwangalia.

Alisema suala la asilimia 16 lipo muda mrefu hata kabla ya sheria mpya kutungwa.

Tajiri huyo ambaye amewekeza Dola 500 milioni za Marekani (zaidi ya Sh1.1 trilioni) nchini anaona sheria hiyo haitendi haki na itawakimbiza wawekezaji.

“Rais Magufuli anapaswa kulitaza hili kwa umakini,” alisema.

Baada ya kuisoma habari hiyo iliyoripotiwa kutoka Uingereza, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo), Dk Hassan Abbasi alisema Serikali inaheshimu maoni ya Dangote na akafafanua kuwa kinachofanyika ni kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

“Iwapo kutakuwa na changamoto zozote Serikali itazungumza na wadau wa sekta husika. Lengo la Serikali si kuwatisha, bali kuwawezesha wawekezaji kufuata na kutii sheria za nchi,” alisema msemaji huyo wa Serikali.

Miaka miwili tangu aingie Ikulu, Rais Magufuli amefanya mambo mengi kutetea rasilimali za nchi na kuhamasisha uwajibikaji serikalini.

Mkakati wake wa kupambana na wizi, rushwa na urasimu umeungwa mkono na watu wengi.

Miongoni mwa hatua alizozichukua ni pamoja na kuboresha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kupambana na dawa za kulevya.

Uthubutu wake wa kuwataka wafanyabiashara wakubwa kulipa kodi wanazostahili umeifanya Mamlaka ya Mapato kuweka rekodi ya makusanyo makubwa kwa mwezi ikifikisha zaidi ya Sh1.4 trilioni.

Ni katika harakati hizo, Rais aliunda tume mbili za kuchunguza uchimbaji, usafirishaji na biashara ya madini ambazo matokeo yake yaliweka wazi udanganyifu unaofanywa kwenye sekta hiyo ambao unalipotezea Taifa mapato mengi linayostahili.

Matokeo ya juhudi hizo yaliifanya TRA iiandikie madai ya Dola190 bilioni za Marekani Kampuni ya Acacia iliyoorodheshwa kwenye Soko la Hisa London (LSE) na Dar es Salaam (DSE). Kiasi hicho kinajumuisha kodi iliyokwepwa, riba na faini kwa takriban miaka 20 tangu ianze kuchimba dhahabu na kusafirisha mchanga nje ya nchi.

Hata hivyo, mazungumzo bado yanaendelea kati ya Serikali na Acacia tangu yalipoanza Julai 31 kusaka muafaka baina ya pande hizo na biashara iendelee kama kawaida.

Licha ya wananchi, jumuiya ya kimataifa na wawekezaji kumpongeza Rais kwa hatua hizo, Dangote anaona si haki kwa Serikali kuwa na asilimia 16 ya hisa bila kulipa chochote.

“Ni kuwazunguka wawekezaji. Miaka ijayo Serikali inaweza ikachukua hisa nyingi zaidi kwa bei ya kujipangia,” alikaririwa Dangote na kuongeza:

“Ingawa ni sheria iliyopitishwa na Bunge, ni mbovu. Ukimfukuza mwekezaji huwezi kumrudisha.”