Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 11:40 am

NEWS: ATIWA MBARONI KWA UTAPELI

KILIMANJARO: Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro kwa ushirikiano na raia wema wamefanikiwa kumtia mbaroni kijana mmoja ambaye amekuwa akitapeli wafanyabiashara katika mikoa ya Manyara,Arusha na Kilimanjaro kwa kutumia jina la kampuni ya vinywaji baridi ya jamii ya Coca cola ya Bonite na kujipatia fedha visivyo halali.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mtaa wa Miembeni kata ya Majengo katika manispaa ya Moshi wameieleza ITV jinsi kijana huyo Joseph Mapunda mkazi wa Njoro katika Manispaa hiyo alivyotaka kujipatia fedha hizo kabla ya kutiwa mbaroni na mwingine Bi Catherine Raphael alifanikiwa kumtapeli jokofu la kuhifadhia soda.

Bi Jasmini amesema, kijana huyo alipokuja dukani kwake alitaka kujua kama mkataba wa kumiliki jokofu umemalizika ili amletee mkataba mwingine wa kupata jokofu hilo kwa sharti la kutoa shs.20,000/= na ndipo alimpotilia mashaka.

Corlman Kimei amewataka wafanyabiashara mkoani Kilimanjaro kuwa makini na watu wa aina hiyo kwa kuwa kampuni inatoa majokofu,meza na viti bila malipo kwa vigezo maalum vilivyopo kwenye mikataba halali ya kampuni hiyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro Kamishna Msaidizi wa Polisi khamisi Issa amewataka wafanyabiashara waliotapeliwa na kijana huyo katika mikoa ya Manyara, Arusha na kilimanjaro kwenda kituo cha polisi majengo kumtambua mtuhumiwa ili wamfungulie mashtaka.

Kamanda Issa pia ametumia nafasi kuwatahadharisha wananchi juu ya kuwepo kwa watu wa aina hiyo wanaotumia majina ya kampuni ya umeme TANESCO na mamlaka ya maji, na usafi wa mazingira (MUWSA) maarufu kwa jina la vishoka na kwamba jeshi la Polisi litaendesha msako mkali wa vishoka.