Home | Terms & Conditions | Help

November 26, 2024, 7:25 pm

NEWS: AFRIKA KUSINI KUENZI MAKABURI YA WAPIGANIA UKOMBOZI KONGWA

DODOMA: Kumbukumbu ya Makaburi ya wapigania uhuru kutoka nchi mbalimbali za Afrika hususani nchi za kusini mwa Afrika waliopoteza maisha katika vita vya ukombozi wa Bara la Afrika yaliyopo wilaya ya Kongwa nchini Tanzania huenda ikatoweka baada ya maeneo hayo kutotuzwa licha ya kuwa mashujaa hao walizisaidia nchi zao kupata uhuru.


Akizungumza mbele ya ujumbe kutoka Afrika Kusini ukiongozwa na wenyeji wao wa Tanzania, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kongwa White Zuberi amesema kuwa mara kaadha amekuwa akipokea ugeni kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao wanakuja kwa lengo la kuona makaburi ya mashujaa wao wa ukombozi lakini bado hawaoni umuhimu wa kuyahifadhi na kuyatunza kwa ajili ya kuyaenzi kwa manufaa ya vizazi vijavyo.


Ujumbe huo kutoka Afrika Kusini ukiongozwa na Mziwonke Dlabantu umesema kuwa ili kutambua mchango wa Tanzania katika kuisaidia nchi hiyo kupata uhuru watahakikisha maeneo yote yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa nchi yao yanaenziwa na kutunzwa ili kumbukumbu hiyo muhimu isipotee.


Ujio wa ujumbe huo unatokana na muendelezo wa program ya urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika wenye lengo la kutambua na kuhifadhi kumbukumbu za harakati za kutafuta uhuru wa nchi za Afrika ambapo nchi ya Tanzania ilishiriki katika kutoa msaada kwa nchi hizo.


Katibu mkuu wizara ya habari, Utamaduni, Sanaa na michezo nchini Tanzania Profesa Elisante Gabriel amesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni(UNESCO) limeridhia kujenga kituo cha kitaifa mkoani Dodoma kwa ajili ya makumbusho ya urithi wa ukombozi ili kuhifadhi historia hiyo muhimu kwa Bara la Afrika.


Wilaya ya Kongwa ni moja ya maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa Bara la Afrika ambapo yanapatikana makaburi ya wapigania uhuru walipoteza maisha wakati wa vita vya ukombozi pamoja na handaki la kijeshi lililotumiwa na Rais wa Msumbiji Samora Machel kwa ajili ya kujificha pamoja na kupatia mafunzo.