Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 5:28 am

NEWS: AFARIKI DUNIA KWA MGANGA WA KIYENYEJI AKIONGEZEWA NGUVU ZA KIUME

SHINYANGA: MWANAUME anayefahamika kwa jina la Joseph Sahni (60), mkazi wa Kijiji cha Nzonza Kata ya Salawe Shinyanga Vijijini, amefariki dunia akiwa nyumbani kwa mganga wa kienyeji wakati akipatiwa matibabu ya nguvu za kiume.


Alikutwa na mauti baada ya kuwekewa dawa aina ya unga kwenye tundu la sehemu zake za siri, kisha kusukumiziwa kwa kupampiwa na pampu ya baiskeli, hivyo kupoteza maisha.

Tukio hilo lilitokea Jumapili saa 10:00 jioni, ambapo Sahni baada ya kupatiwa matibabu hayo, alianza kutokwa damu nyingi sehemu zake za siri kisha kuishiwa nguvu na kupoteza maisha.

Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Simon Haule, alisema Jeshi lake linamshikilia mtuhumiwa mganga huyo wa kienyeji, Robert Mkoma, kwa tuhuma za mauaji, na baadaye atafikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika.

“Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuacha tabia ya kuendekeza kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kutafuta tiba, waende kwenye vituo vya afya au hospitali kufanyiwa uangalizi na kupewa matibabu sahihi,” alisema Kamanda Haule.

Katika tukio lingine, Jeshi hilo linamsaka Masesa Sesaguli, mkazi wa Kijiji cha Mwakolongwa Tarafa ya Itwangi Shinyanga Vijijini, kwa tuhuma za kumuua binti yake, Nshoma Masesa (16), aliyekuwa akisoma kidato cha pili Buhongwa jijini Mwanza, baada ya kuacha masomo na kwenda kuolewa wilayani Kahama.

Kamanda Haule alisema baada ya binti huyo kutafutwa na kurejeshwa nyumbani kwao, ndipo baba yake alianza kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili hadi kuishiwa nguvu na kupoteza maisha.

Kamanda Haule alisema baada ya mauaji hayo, mwanaume huyo alitorokea kusikojulikana.

Kamanda Haule aliwaasa wanafunzi wa kike kujikita zaidi kupenda masomo, ili kutimiza malengo yao, na kuacha tabia ya kujiingiza kwenye masuala ya mapenzi katika umri mdogo, ambayo yamekuwa yakiwaharibia mwelekeo wa maisha yao.