Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 7:25 pm

NEWS: ACT KUWAAJIBISHA WABUNGE WA CCM WALIOTAMANI ZITTO KUUWAWA

Dar es Salaam. Naibu Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT - Wazalendo, Juma Duni Haji amesema chama chao kimechukulia kwa uzito mkubwa vitisho vilivyotolewa na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe Bungeni Mjini Dodoma.

Duni ametoa kauli hiyo leo Jumapili Februari 2, 2020 Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari akizungumzia barua ambayo Zitto aliwaandikia Benki Kuu (WB) kusitisha kutoa mkopo kwa Serikali ya Tanzania.

Amesema tayari chama kimewaelekeza mawakili wake kuliangalia suala hilo huku wakitoa onyo kwamba chochote kitakachomtokea Zitto basi wabunge hao waliomtishia maisha watawajibika kikamilifu.

“Chama cha ACT Wazalendo kimevichukulia kwa uzito mkubwa vitisho vya wabunge wa CCM dhidi ya kiongozi wetu, Zitto Kabwe.

“Tunawaeleza kuwa lolote lile baya litakalomkuta, watawajibika kikamilifu. Chama chetu kimewaweka katika tahadhari wanachama wetu nchi nzima kumlinda kiongozi wao kwa lolote,” amesema Duni.

Kiongozi huyo amesema chama hicho kinampongeza Zitto kwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za watoto wa kike wanaopata mimba kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua.

Amefafanua kwamba barua ya Zitto haina nia yoyote ovu bali alitaka mkopo utolewe kwa Tanzania baada ya changamoto mbalimbali kama vile ukiukaji wa haki za binadamu ziwe zimetatuliwa.

“Tumesikitishwa na tumefadhaishwa na matumizi mabaya ya Bunge dhidi ya kiongozi wetu wa chama, tunachukulia kila neno lililotoka kwa tahadhari kubwa," amesema.