Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 4:27 pm

MICHAEL WAMBURA: NIMEKIRI KWA DPP NA KUOMBA MSAMAHA

Dar es Salaam. Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu kuwa ameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa yake.

Wambura alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Februari 11, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya Sh 100milioni, katika kesi ya uhujumu uchumi namba 10/2019.

Wambura alidai hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa aliandika barua kwa DPP ili kuomba msamaha na kukiri makosa yake hivyo aliuomba upande wa mashtaka kufuatilia ili aweze kupata haki yake.

"Niliandika barua kwa DPP ili kuomba msamaha na kukiri makosa yangu hivyo ninasubiri majibu,"alidai Wambura.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai suala hilo analifanyia kazi kwa haraka zaidi

Baada ya maelezo hayo Mhina aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 16, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.


Katika shtaka la kwanza ambalo ni la kughushi, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 6, 2004, sehemu isiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam.



Siku hiyo, Wambura kwa nia ya kutapeli alitengeneza barua ya kughushi ambayo haina kumbu kumbu namba akionyesha imeandikwa na E Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Jeck system anadai kurejeshewa malipo ya mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba aliyokuwa ameikopesha TFF.


Katika shtaka la kutoa na kuwasilisha nyaraka ya uongo, mshtakiwa alitoa barua iliyokuwa haina kumbu kumbu namba ya Julai 6, 2004, akijifanya kwamba ni barua iliyoandikwa na E. Maganga ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Jeck System Ltd, akionyesha kuwa anadai mkopo wa USD 30,000 pamoja na riba waliokopeshwa TFF huku akijua kuwa siyo kweli.

Hata hivyo, kuanzia shtaka la tatu hadi la 15 mshtakiwa anadaiwa kujipatia kiasi cha zaidi Sh 95 milioni, kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya jumla ya kiasi cha fedha mbali mbali na riba kutoka kwa kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa siyo kweli.

Pia, katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Wambura anadiawa kutenda kosa hilo, Juni 17, 2015 huko katika ofisi za TFF, ambapo kwa njia ya udanganyifu, mshtakiwa alijipayia Sh 10milioni kutoka TFF kwa kuonesha kuwa ni malipo ya USD 30,000 pamoja na riba kutoka kwenye kampuni hiyo ha Jeck jambo ambalo siyo kweli.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Wambura anadai, kati ya Agosti 15 na Oktoba 21, 2014, makao makuu ya Shirikisho hilo, alijipatia Sh 25milioni kutoka TFF huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.