Home | Terms & Conditions | Help

November 24, 2024, 2:55 pm

MAKALA: UKIANGUKA USIKATE TAMAA, UNAWEZA KUSIMAMA TENA.

“Kuna wakati nilipitia majaribu na kujihisi sina haki wala amani , dunia ilinitenga na wala hakukuwa na mtu wa kunisikiliza wala kuniamini kwa chochote lakini ilifika wakati niliweza kuamka na kusimama tena”anasema Endre Kalebi Chota kijana ambaye alianguka na kusimama tena.

Kijana huyu Andrew anatukumbusha kuwa ukianguka huna haja ya kukata tamaa wala kubaki hapo chini ulipo baada ya kuanguka majaribuni kwani kuna msaada mwingine juu ya maisha yako ya mateso.

“Hakuna mkamilifu duniani lakini kuna wakati mioyo yetu imekuwa ikitusaliti kwa kutuchochea kufanya vitu visivyoendana na maadili ya dini zetu”anazidi kusisitiza kijana huyu mwenye mvuto wa kiimani.

Hata hivyo kijana huyu anatukumbusha kuwa pamoja na kwamba hakuna mkamilifu duniani ,ni lazima maamuzi yetu tunayoyafanya yaendane na maadili yetu bila kujali kuiridhisha mioyo yetu kwani wakati mwingine moyo huwa mdanganyifu na hukubali kutusaliti.

Hata hivyo anasema kuwa uwezo wa Mwenyezi mungu unaweza kugeuza kisiki kilichokuangusha na kuwa kigogo cha kukuvushia kwenye ushindi na kuwa mtu mwingine hapa duniani.

Usijali wangapi wanakucheka ,wangapi wamekuumiza na kubwa kuliko vyote usiangalie watu watakufikiriaje .Yote kwa yote ni kuamgalia wapi ulipojikwaa na kuangua ili ujue wapi pa kuanzia.

Kijana huyu Endrew aliwahi kuanguka na kutengwa na jamii yake ambapo alipitia kipindi kigumu na alihisiwa kuwa ni jalala la kila baya ,unajua ni kwa sababu gani?

Pamoja na kwamba mara nyingi tunakumbushwa kuwa akili ya kuambiwa changanya na ya kwako,lakini mara nyingi binadamu hujikuta akisikiliza upande mwingine na kuamua zinamtuma kufanya nini.

Hapa nazungumzia marafiki ,mara nyingi tunajikuta tukishinikizwa na marafiki zetu kufanya mambo mabalimbali nasi tukashawishika bila kuangalia madhara yatakayo tokea hapo badae.

Na hapo ndipo tunapaswa kuwa na macho ya rohoni ili kuweza kuona maono ya maisha yetu,kwani tunaambiwa kwamba pasipo na maono unaweza kuangamia.

Awali,Kijana huyu anasema kuwa aliweza kuwaamini sana marafiki kuliko hata ndugu zake wa damu,lakini aligundua kuwa anapotea,anasisitiza kuwa pamoja na kuwa tunapaswa kuwapa watu wengine nafasi za kuwaamini ni lazima tuwe tunamshirikisha Mwenyezi Mungu juu ya nani wa kumwamini na wakati gani.

“Ni lazima tuwape nafasi watu wengine ya kuwaamini lakini kwa kumshirikisha mwenyezi Mungu,kwani kuna marafiki hatupaswi kuwaamini kabisa”anasema.

Isitoshe kusema hayo pekee ,bali Endrew anasema kuwa pamoja na kuwa hatupaswi kumwamini kila mtu vile vile tunapaswa kuitumia nafasi hiyo kuwabadilisha wengine na kuwafanya wasimame tena ili wafanane nasi.

Kutokana na ukweli uliopo kuwa kuna wakati tunaanguka kwa kupotoshwa na marafiki,mwanasaikolojia mmoja makini Dk.Paul Matemu anajaribu kutufundisha aina za marafiki tunazopaswa kuwa nazo ikiwa ni pamoja na ubora wao.

“Kuna watu wamepoteza utu wao kwa sababu ya marafiki wabaya na wengine kuumizwa na marafiki wanafiki ,unapaswa kuwa na macho ya rohoni kuepuka usumbufu wa kurua makosa”anasema Matemu.

Dk.Matemu anaorodhesha makundi matatu ya marafiki ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kukusaidia katika usalama wa furaha ya maisha yako.

Anasema kuwa Kundi la kwa kwanza la marafiki, ni wale marafiki ni wale wanaokupenda kwa dhati ya moyo bila masharti (Confidants)hukubali kuwa nawe ukiwa umeanguka au umesimama ,ukiwa tajiri au hata katika hali ya umasikini.

Aina hii ya urafiki huwa haiangalii kama uko sahihi ama umekosea ,aina hii hujali zaidi hisia zako na kukubali kulia pale unapolia na kukuelewa muda wote ambapo unapaswa kuwa huru kuwaeleza hisia zote .

Hata hivyo mwanasaikolojia huyu anazidi kubainisha aina nyingine ya urafiki kuwa ni kundi la marafiki hatari(Constituents),marafiki hawa hawako tayari kukuona unafanikiwa ,wako kwa ajili ya kuiba maono yako .

“Marafiki ambao wako kwa ajili ya kuiba maono yako ni hatari sana kwani pasipo maono watu huangamia na rafiki huyu yupo tayari kukuangamiza wakati wowote na anaweza kujitoa kwa ajili ya kukuumiza”anasisitiza Matemu.

Mbali na hayo anasema marafiki wa aina hii huhitaji kile unachokitaka na hivyo ni rahisi sana kukuumiza bila kujali hisia zako na hivyo unapaswa kusimama imara katika kutetea maono yako.

Pamoja na hayo anabainisha kundi lingine kuwa ni la marafiki ambao huletwa ama husogezwa na mwenyezi Mungu katika ukaribu wa maisha yetu kwa kusudi maalumu na wakati mwingine kwa muda maalumu tu na baadaye hutoweka .

Kundi hili linabeba watu wenye utayari wa kupigana na kile unachokipigania ili kukusaidia kukipata na kuonesha ushindi katika maisha yako na baada ya hapo hutawaona tena.

“Hii haimaanishi kuwa wamekuacha,hapana..marafiki hawa wanakuwepo wakati wa shida zako tu ili kukusaidia ushinde na hivyo hupaswi kuwalaumu kwa nini wameondoka kumbuka wameondoka sio wamekuacha”anasema Dk.Matemu .

Hata hivyo Matemu anatoa angalizo kuwa kuna marafiki wengine hawako kwenye kundi lolote kati ya hayo ambapo ukiwa nao hutakuwa na malengo katika maisha yako na hutaweza kufikia malengo na unachotakiwa kukifanya ni kujitenga nao.

Hivyo basi ,kwa kuzingatia makundi hayo ya urafiki unaweza kuchagua yupi ni sahihi kwako kwa kuangalia mapenzi wanayoyaonesha kwako kwa vitendo japo unatakiwa kuwa makini kwa kuwa wengine huficha makucha yao.

Pia unapaswa kuangalia wapi ulipokosea mara ya kwanza mpaka ukaanguka majaribuni ikiwa ni pamoja na kuchunguza njia zako ili uendelee na safari.

Kamwe usikubali kushindwa kirahisi hata kama ukianguka mara nyingi zaidi japo unapaswa kuomba mwongozo kwa Mungu ili aweze kuwa msaada sahihi kwako katika kuyashinda majaribu .

Pengine huwezi kuendelea tena kwa namna hali inavyoonekena sasa,lakini unakumbushwa kuwa unaweza kufanya vizuri zaidi hata baada ya kuwa umeshindwa mara nyingi na jamii kukuona usie na maana tena.

Kumbuka umeumbwa na Mungu na hivyo upo duniani kwa sababu,jikumbushe mara kwa mara kuwa huko kama wanavyosema ,wao sio hatma ya maisha yako japo ni kweli umeanguka unahitaji nafasi nyingine kwa kuwa kila mmoja anahitaji nafasi kwa mara nyingi zaidi ili kujirekebisha.

Jihadhali usiyape ushindi yale mabaya yanayozungumza juu yako bali simama na ujipange sawasawa kwa ajili yakupigana na wanaoteta nawe bila kujali utatumia muda gani,au utakutana na nini katika mapambano angalia msaada wako Ni mwenyezi mungu na kutokubali kuchezea hisia za watu wengine.