Home | Terms & Conditions | Help

November 27, 2024, 9:29 am

GOOGLE BOY" MTOTO ANAYEJIBU MASWALI YA KITAALAM KWA USAHIHI

Kautilya Pandit maarufu Google Boy, ni Raia wa India mwenye uwezo mkubwa wa AKILI NA FIKRA , anaumri wa miaka 10 kwasasa lakini tayari anajua kila kitu muhimu kama msomi wa kawaida Duniani, anauwezo wa kuchambua Pato la Ndani la Taifa (GDP) la India na Australia, anauwezo wa kuzungumzia siasa za Indonesia kwa usahihi kabisa.

Huko Kohand, katika Kijiji cha Karnal, Jimbo la Haryana nchini India, Kautilya tangu akiwa na miaka mitano (2013), tayari alishaanza kujulikana kama ‘Google Boy’ au Encyclopedia inayotembea.

Majina hayo ya utani yanamaanisha kitu chochote ambacho unaweza kukitafuta mtandaoni kama google tayari kipo ndani ya kichwa cha mvulana huyo mwenye umri wa miaka minane.

Wazazi wake wanasema, mtoto huyo tangu akiwa mdogo alikuwa mtu wa kuwarushia maswali ya hapa na pale kuhusu chochote kinachomjia kichwani au kukiona mbele yake.

Kutokana na wakati mwingine kuwatia hofu wazazi wake, walilazimika kwenda kitengo cha saikolojia cha Chuo Kikuu cha Kurukshetra.

Baada ya uchunguzi, waliambiwa IQ ya mtoto wao huyo inasimama katika pointi 130 dhidi ya 92-110 za mtoto wa kawaida na hivyo anapaswa kupewa uangalizi maalumu kielimu.

Kiwango hicho cha IQ ni sawa na kile cha mwanafizikia maarufu Albert Einstein.

“Mtoto huyu mwenye akili Kautilya Pandit, mwenye umri wa miaka mitano tu (2013) anajibu maswali mengi, ambayo wanasayansi na watu wenye maarifa hawawezi kuyajibu,” msanii maarufu nchini India Amitah Bachchan aliandika katika akaunti yake ya Twitter usiku wa Oktoba 25, 2013 baada ya kurekodi kipindi cha televisheni kilichomhusisha Pandit mjini Mumbai.

Katika kipindi hicho, Kautilya aliwashangaza wengi kwa kuchukua sekunde tu kujibu kila swali lililoelekezwa kwake kwa usahihi kabisa.

Kwao Kohand, kwa sasa ni mtu maarufu. “Watu wengi hujitokeza kumtembelea nyumbani kila siku na kupiga naye picha,” anasema baba yake Satish Sharma, ambaye anaendesha shule binafsi kijijini hapo.

Sharma anasema pamoja na kipaji cha mwanawe, ni mtu anayependa kujifunza kila kitu ikiwamo mataifa duniani na ulimwengu kwa ujumla wake.

Yote hayo Sharma anasema alianza kumgundua wakati akiwa na umri wa miaka mitano.

Ilianza kwa yeye kama mwalimu kuwataka na kuwatia moyo watoto wa shule yake wafanye jaribio la kuvunja rekodi iliyowekwa na msichana mmoja mdogo wa Ulaya aliyeweza kuonesha nchi 150 katika ramani ya dunia.

“Niliwataka watoto wote kuleta shuleni atlas ili waweze kufundishwa maeneo ya nchi mbalimbali. Kufikia jioni ya siku iliyofuata, upande wa Kautilya aliweza kuiweka kichwani ramani nzima ya dunia. Siku 20 baadaye aliijua atlasi kama kiganja cha mkono wake,” anasema Sharma.