Home | Terms & Conditions | Help

November 25, 2024, 11:45 am

CHAMA CHA ACT CHAMTAKA JAFO KUONDOA HUJUMA UCHAGUZI SEREKAILI ZA MTAA

CHAMA cha ACT Wazalendo Kimemtaka Waziri wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Sulemani Jafo kuziondoa mara moja njama ovu na hujuma zinazofanywe na watendaji wa kata kwenye zoezi la uchaguzi wa serekali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Mnamo Novemba 24 mwaka huu.

Akizungumza leo Novemba 1,2019 jijini Dar es Salaam Mratibu wa Mawasiliano Taifa wa Chama cha ACT, Mbarala Maharagande amesema kuwa Waziri Sulemani Jafo anapaswa kutambua kuwa kuna njama ovu na hujuma dhidi ya vyama vya upinzani kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa unaoelekea kufanyika.

"Kuna tofauti kati ya hujuma au njama ovu na dosari au mapungufu, hujuma na njama ovu hizi zinafanywa dhidi ya vyama vya upinzani na wagombea wake pekee na hakuna lalamiko hata moja tulilolisikia au kushuhudia kutoka kwa CCM nchi nzima. Hii maana yake ni kwamba huenda hujuma hizo zinaratibiwa na Ofisi yake na wala hazitokei kwa bahati mbaya,"amesema Maharagande.

Amesema kuwa dosari zilizopo ofisi zinazosimamia uchakuguzi huo ikiwa ni kutokuwa na mihuri, kufungwa kwa ofisi, wagombea kutokupewa nakala za fomu za kugombea katika vijiji, kata na vitongoji. Ametaja maeneo yenye dosari hizo ambazo ni Ruangwa, Liwale, Bukombe, Songwe, Tabora, Busanda, Misungwi, Moshi Mjini, Morogoro Kusini Mashariki, Kasulu Vijijini, Tanga, Dar es Salaam, Newala, Mkoa wa Pwani na Mbeya.

"Tangu mchakato wa uchukuaji wa fomu uanze tarehe Oktoba 29, 2019 wanachama 276,401 wamejitokeza nchini kote kugombea nafasi za uongozi kupitia ACT-Wazalendo huku idadi hiyo ikiongezeka siku hadi siku na miongoni mwao kufanikiwa kuchukua fomu za kugombea". Amesema Maharagande.

Pia Maharagande amesema Waziri Jafo achukue hatua dhidi ya viongozi watakaokiuka kanuni, taratibu, sheria na miongozo ya usimamizi wa uchaguzi.Hata hivyo amewaasa viongozi wa dini na wastaafu kuhimiza kutenda kwa Haki na kukemea viashiria vya kupotea kwa amani na utulivu kwani amani ni tunda la haki na pia kuamrisha kutenda mema kuendelea kukataza maovu.

Kwa upande wake Katibu wa Programu za Jamii Taifa wa ACT Mwanaharusi Bunduki amewashauri wasimamizi wa uchaguzi kupitia Serikali kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na miongozo ya kusimamia uchaguzi hiyo ili kuendelea kuitunza amani ya nchi.